Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MISWADA YA MAREKEBISHO YA SHERIA YAWASILISHWA MBELE YA KAMATI

Imewekwa: 12 Aug, 2026
MISWADA YA MAREKEBISHO YA SHERIA YAWASILISHWA MBELE YA KAMATI

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, ameipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kwa miongozo na ushauri unaochangia kuharakisha mchakato wa maboresho ya sheria mbalimbali ili ziendane na wakati na mahitaji ya maendeleo ya Taifa.

Dkt. Homera ametoa pongezi hizo leo, Agosti 11, 2026, wakati akitoa maneno ya utangulizi kabla ya uwasilishaji wa mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali yaliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, kwa ajili ya kufanyiwa mapitio na Kamati hiyo katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Bunge, jijini Dodoma.

Amesema miongozo inayotolewa na Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb), imekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha sheria zinaendelea kuboreshwa na kuwa wezeshi katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.

Amesema maboresho hayo ya sheria ni muhimu katika kuweka mazingira bora ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akiiahidi kamati kuwa Wizara  itaendelea   kushirikiana na Kamati hiyo katika kufanikisha utekelezaji wa Dira 2050.

Mapendekezo hayo ya marekebisho ya sheria yanatarajiwa kuwasilishwa Bungeni hivi karibuni na yanahusu maeneo muhimu ya maendeleo, usalama na usimamizi wa rasilimali za Taifa.

Sheria zinazopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni pamoja na Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (Sura ya 116), Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka ya Wilaya) (Sura ya 287), Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) (Sura ya 288), Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa (Sura ya 61), Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini (Sura ya 138), pamoja na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori (Sura ya 283).

Marekebisho hayo yanatarajiwa kuimarisha zaidi misingi ya kisheria katika maeneo mbalimbali, ikiwemo matumizi ya ardhi, uendeshaji wa Serikali za Mitaa, usalama wa Taifa, uthamini na usajili wa wathamini, pamoja na uhifadhi wa wanyamapori.