Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mkandarasi wa jengo la Mashtaka Mbeya kuchukuliwa hatua

Imewekwa: 03 Apr, 2023
Mkandarasi wa jengo la Mashtaka Mbeya kuchukuliwa hatua

Na Felix Chakila & Lusajo Mwakabuku.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameelekeza hatua za kisheria kuchukuliwa kwa kuzingatia masharti ya mkataba kwa Mkandarasi anayejenga Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ya Mkoa wa Mbeya iwapo atashindwa kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo ifikapo 20 Aprili, 2023.

Mheshimiwa Ndumbaro ametoa maelekezo hayo baada ya kufanya ukaguzi na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo katika jiji la Mbeya, tarehe 01 Aprili, 2023 alipokuwa kwenye ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa Ofisi za Mashtaka katika Mikoa ya Mbeya na Rukwa ikiwa ni sehemu ya miradi inayoendelea kutekelezwa nchi nzima kwa lengo la kusogeza huduma karibu zaidi kwa jamii.

Katika ukaguzi huo, Mhe. Ndumbaro alibaini kuwa utekelezaji wa mradi huo umepitiliza muda wake bila sababu za msingi hivyo akamwambia Mkandarasi kuwa Serikali haitokua tayari kuongeza muda wa ziada baada ya tarehe 20 Aprili, 2023 na badala yake hatua za kisheria zitachukuliwa kutokana na kukiukwa kwa vipengele vya mkataba wa makubaliano ya kazi hiyo.

Katika hatua nyingine Dkt. Ndumbaro amekagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Rukwa ambapo Mkandarasi huyo mzawa ndiye anayejenga jengo la Mkoa wa Katavi, ambaye hapo napo ujenzi wake umefikia asilimia 35 tu.

Mhe. Ndumbaro amemwelekeza Mkandarasi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili kuwawezesha watumishi ambao wapo katika majengo ya kupanga wanahamia katika majengo hayo na kuokoa fedha za Serikali za kugharamia pango.

Aidha, Mheshimiwa Ndumbaro alisema kuwa Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa Wakandarasi wa ndani hivyo ni wajibu wao kuiaminisha Serikali kuwa wanaweza kutimiza majukumu yao kwa ufanisi na kwa wakati ili Wakandarasi hawa wazawa waweze kuendelea kuaminika.

Ziara hii katika Mikoa ya Mbeya na Rukwa ni sehemu ya ziara za Mhe. Ndumbaro za ukaguzi wa ujenzi wa Ofisi za Taifa za Mashtaka unaoendelea katika mikoa mbalimbali nchini.