Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MoCLA Yaombwa Kuongeza Ushirikiano na Wazee Wa Kimila na Viongozi wa Dini

Imewekwa: 07 Aug, 2023
MoCLA Yaombwa Kuongeza Ushirikiano na Wazee Wa Kimila na Viongozi wa Dini

Na Lusajo Mwakabuku – WKS Babati

Wazee wa Kimila wa Viongozi wa Dini wametoa wito kwa uongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria kuongeza ukaribu na Viongozi hao kwani wao ndio wapo karibu na jamii katika masuala ya malezi kwa watoto na vijana kimaadili ili kuweka mustakabali wa Taifa na watu wake kwenye mikono salama.

Wazee na viongozi hao wameyasema hayo tarehe 07/08/2023 katika warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi hao kwenye masuala ya kisheria katika majukumu yao ya kila siku hususan kwenye kufanya usuluhishi wa migogoro mbalimbali na kudhibiti vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

Wakiongea wakati wa majadiliano baada ya kutolewa mada mbalimbali kutoka kwa wataalam wa sheria kutoka wizarani na taasisi binafsi, wazee hao walibainisha kuwa wao wapo karibu na wananchi na kila siku wanakutana na mambo mengi ambayo mengine yanapaswa kupatiwa ufumbuzi katika ngazi ya Wizara na hivyo kukiwa na ushirikiano wa karibu kutarahisisha utatuzi wa migogoro na kuipunguzia Mahakama mzigo wa kesi.

“Sisi tunakutana na wananchi wetu katika maeneo yetu angalau kila wiki hasa Viongozi wetu wa Dini ambao kila Jumapili kwa wakristu na Ijumaa kwa Waislam tunapata nafasi ya kusikiliza na kutatua kero nyingi na sisi tunakuwa na taarifa nyingi ambazo Wizara ikizipata inaweza kuwa katika sehemu nzuri zaidi ya kuboresha usimamizi wa haki” Alisema Chifu Mkuu wa Wamasai Tanzania Isack Olekisongo Meijo.

Aidha, Chief Meijo aliongeza kuwa vijana wakifundishwa vizuri mila, desturi na maelezo ya kitaalam kutoka kwa wataalam huku wakikumbushwa kushika mafundisho ya dini na wakawa na hofu ya Mungu maovu mengi ikiwemo ndoa za jinsia moja, ulawiti na unyanyasaji wa kijinsia vitapungua kwa kiwango kikubwa hapa nchini.

Akiongelea madhumuni ya kuitisha warsha hiyo, Wakili wa serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria George Mollel alisema Serikali inatambua umuhimu wa madhehebu ya Dini na Viongozi wa Dini kuwa ni sehemu muhimu katika kuimarisha amani katika jamii na ndio maana Serikali inaendelea kushirikiana nao katika kujenga maadili mema kuanzia ngazi ya familia na jamii kwa ujumla.

Mwanasheria kutoka shirika la watoa msaada wa kisheria linalojulikana kwa jina la CSP bwana Eliakim Paulo akitoa elimu ya jinsi sheria za nchi zinavyotekelezwa kwa viongozi hao alisema elimu inayotolewa kwa wazee hao itatumika kuwasaidia katika kuleta mabadiliko kwenye jamii zao ikiwemo kupambana na ukatili wa kijinsia, kuchochea usawa wa kijinsia, kusomesha watoto wa kike na wanawake kushiriki kwenye shughuli za kimaendeleo.