Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MoCLA Yazindua Kituo cha Huduma kwa Mteja

Imewekwa: 11 Sep, 2024
MoCLA Yazindua Kituo cha Huduma kwa Mteja

Hyasinta Kissima – WyKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria  Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema Wizara yake imepanua wigo wa kuhudumia wananchi bila kuwalazimu kufika ofisi za Wizara kupitia Kituo cha Huduma  kwa Mteja.

Hafla ya kuzindua rasmi kituo hicho imefanyika tarehe 05 Septemba, 2024 Ofisi za Wizara Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma ambapo yeye alikuwa Mgeni Rasmi.

“Kupitia namba ya simu 026 216 0360 mwananchi anaweza kuwasilisha lalamiko lake na lalamiko hilo kufanyiwa kazi kwa wakati na kwa ufanisi bila mwananchi kulazimika kufika ofisi za Wizara. Huduma hii inasaidia kuwafikia wananchi wengi hususan wasio na uwezo wa kumudu gharama za usafiri kuja kuwasilisha malalamiko yao wizarani.” Alisema.

Wizara imeanzisha kituo hicho kupitia Programu ya Kujenga Uwezo wa Taasisi katika Kupambana na Rushwa (Building Sustainable Anti-Corruption Action in Tanzania – BSAAT) ili kupokea taarifa na malalamiko yanayohusu tuhuma za rushwa, ukiukwaji wa haki unaofanywa na taasisi ama mtu mmoja mmoja na maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusiana na huduma zinazotolewa na Wizara pamoja na Taasisi zote zilizo katika mnyororo wa utoaji haki.

Kituo hicho kimeanza kufanya kazi mwezi Februari, 2024 na hadi kufikia tarehe 31 Agosti, 2024 jumla ya malalamiko 499 yamesajiliwa, kati ya hayo malalamiko 410 sawa na asilimia 82 yamefanyiwa kazi kwa ukamilifu na 89 sawa na asilimia 18 yako katika hatua mbalimbali ya utekelezaji wake. Kwa sasa Kituo kinafanya kazi masaa yote ya kazi ila upo mpango wa kuongeza muda wa  kutoa huduma kituoni hadi masaa 24 katika siku saba za wiki.

Mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanzishwa kwa kituo hicho ni pamoja na  kupokea malalamiko yanayohusu masuala ya kisheria; Kuratibu upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wasiomudu gharama za wanasheria; Kupokea maoni, mapendekezo na ushauri juu ya huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara; Kupata mrejesho wa namna malalamiko yaliyoshughulikiwa na taasisi mbalimbali; Kuwarahisishia wananchi kufuatilia utekelezaji wa malalamiko yao kwa wakati pasipo kulazimika kufuata huduma hizo wizarani, hivyo kupata nafasi yakufanya shughuli za maendeleo.

Awali akitoa neno la utangulizi kwa niaba ya Katibu Mkuu Bw. Eliakim Maswi, Mkurugenzi wa Idara Katiba na Ufuatiliaji Haki Bi. Jane Lyimo amesema Kituo hicho kimeanzishwa baada ya Wizara kubaini kuwa malalamiko mengi ya wananchi yamekuwa yakiwasilishwa wizarani kwa njia ya barua au wananchi hao kufika moja kwa moja kwenye ofisi za Wizara kwa kutumia gharama kubwa za usafiri na kujikimu.  Vilevile, uwepo wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambayo inaendeshwa na Wizara katika maeneo mbalimbali nchini imeibua uwepo wa malalamiko na hoja mbalimbali za kisheria kwa wananchi ambazo zinahitaji ufumbuzi wa haraka.