Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mradi wa BSAAT na Uboreshaji wa Mfumo wa Haki Jinai Nchini

Imewekwa: 28 Jun, 2024
Mradi wa BSAAT na Uboreshaji wa Mfumo wa Haki Jinai Nchini

William Mabusi – WKS Morogoro

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Beatrice Mpembo amesema Wizara imeendelea kunufaika na Programu ya Kujenga Uwezo wa Taasisi katika Kupambana na Rushwa Nchini (Building Sustainable Anti-Corruption Action in Tanzania - BSAAT) kwa kutekeleza majukumu mbalimbali yanayohusu kuboresha mfumo wa haki jinai nchini.

Bi. Mpembo amesema hayo kwenye kikao cha tathmini ya mradi huo kwa kazi zilizofanywa kwa mwaka 2023/24, tarehe 28 Juni, 2024 mjini Morogoro.

“Wizara ya Katiba na Sheria ni moja ya Taasisi nufaika na mradi wa BSAAT, kupitia programu hiyo Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yanayohusu kuboresha mfumo wa haki jinai nchini ili uweze kuwa na ufanisi na tija katika kushughulikia haki jinai nchini.” Amesema na kuongeza;

“Wizara inatekeleza maeneo matatu katika program hii, maeneo hayo ni Kuimarisha utambuzi wa viashiria vya rushwa kwenye mfumo wa haki jinai vinavyolenga kupunguza motisha kwa watumishi na kujihusisha na masuala ya rushwa; Mfumo wa haki jinai unaolinda na kuharakisha haki za wahalifu, wahanga na mashahidi; Ushahidi wa mifumo mizuri inayopelekea ubora na ufanisi wa uendeshaji mashauri.”

Kupitia mradi huo Wizara imeanzisha Kituo cha Huduma kwa Mteja – Call Center kilichoanza kufanya kazi mwezi Februari, 2024 kikiwa na lengo la kuboresha utoaji huduma kwa wananchi, ikiwemo usikilizaji wa malalamiko yanayohusu rushwa kubwa na kuwasilisha rufaa hizo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa ajili ya uchunguzi. Wateja wanawasiliana na Kituo kwa kupiga simu namba 026 216 0360, kutuma jumbe mbalimbali kupitia WhatsApp namba 0739101910 na e-mail malalamiko@sheria.go.tz.

Mbali na kufanyia kazi masuala yanayohusu rushwa kubwa, kituo hicho pia kinapokea malalamiko mbalimbali yanayohusu masuala ya kisheria na yasiyo ya kisheria na kuyashughulikia ipasavyo.

Mradi huo umeanza kutekelezwa nchini tangu mwaka 2017 ambapo ndani ya Wizara Mradi unatekelezwa kupitia Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki, Idara ya Sera na Mipango na Kitengo cha TEHAMA.