MSLAC Imesaidia Kusukuma Mashauri Mengi ya Jinai – DPP Mwakitalu

Hyasinta Kissima-WKS Njombe
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Sylvester Mwakitalu, amesema kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imesaidia kusukuma mashauri mengi ya jinai kutokana na malalamiko na mapendekezo ambayo wamekuwa wakiyapokea kutoka kwa wadau wao.
Mwakitalu aliyasema hayo mjini Njombe mara baada ya kutembelea katika Gereza la Njombe na kuzungumza na mahabusu na wafungwa waliopo katika Gereza hilo.
"Katika mikoa ambayo kampeni hii imeshafanyika na sasa katika mkoa wa Njombe, tumekwenda kwenye Magereza, tumekwenda kwenye mahabusu za watoto kuna mambo mengi yameibuka na mengi tumeyafanyia kazi. Zipo baadhi ya kesi zimesimama haziendelei, kutokana na sababu mbalimbali lakini baada ya kusikia na kupokea malalamiko na maelekezo kutoka kwa wadau mengi tumeyapatia ufumbuzi."Alisema Mwakitalu
DPP Mwakitalu amesema kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria imesaidia sana kusukuma mashauri mengi ya Jinai kwa wateja wanaowahudumia ikiwa ni pamoja na watuhumiwa, waathirika wa makosa hayo na mashahidi.
Rai imetolewa kwa Wananchi kufika katika Ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka zilizopo katika makao makuu ya Mikoa yote Tanzania Bara na Ofisi katika wilaya 62 kwa ajili ya kupata ushauri na kuwasilisha malalamiko yao katika mashauri mbalimbali ili kupata ushauri wa kitaalamu.