MSLAC Yawafuta Machozi Walioshindwa Kumudu Gharama za Mawakili

Hyasinta Kissima – WKS Njombe
Wananchi wa Kijiji cha Nundu Kata ya Yakobi Halmashauri ya Mji Njombe wamepongeza ujio wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutokana na huduma hiyo kutolewa bila malipo, ambapo awali Wananchi walidhulumiwa haki zao kutokana na wengi kushindwa kumudu gharama za Mawakili.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti mara baada ya timu ya wataalam wa msaada wa kisheria kufika Kijijini hapo kwa lengo la kutoa elimu, baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Nundu wamesema kuwa, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kujipambanua kwa kuendelea kuwajali Wananchi, kuwafuta machozi na kuhakikisha haki inatendeka kwa kila Mtanzania bila kujali kipato cha chake.
"Wakati mwingine katika kudai haki inaweza kufikia hatua unakua haujaridhika na haujui uende wapi. Unaweza kuwa umeingia kwenye mgogoro na mtu mwenye uwezo wa kuwa na Mawakili au taasisi ambayo wapo Wanasheria hivyo unafikia hatua unakosa msaada na haki inapotea. Msaada wa Kisheria wa Mama Samia sisi walala hoi tunaona mwanga" Alisema Innocent Mlange mkazi wa Kijiji cha Nundu.
Bernard Isdory ni mkazi wa Kijiji cha Nundu ambaye yeye aliambatana na shemeji yake (mke wa mdogo wake) akilalamika kuhusu mdogo wake kumtelekeza mkewe na watoto wawili na kuwafukuza katika nyumba waliokuwa wamejenga na kuishi pamoja awali na kwenda kuishi katika Mkoa wa Ruvuma.
Bernard anasema kuwa mara baada ya kuonana na wataalam waliofika kijijini hapo kupitia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, imewajengea uwezo wa namna ya kuendelea na shauri hilo na matarajio yao ni kuona mgogoro huo unafikia muafaka na haki kutendeka.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imeendelea kuwafikia Wananchi katika Kata na Vijiji mbalimbali vya Mkoa wa Njombe ambapo Wananchi mbalimbali wameendelea kujitokeza kuchangamkia fursa hiyo.