Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Naibu Waziri afanya ziara RITA

Imewekwa: 17 Mar, 2023
Naibu Waziri afanya ziara RITA

Na Lusajo Mwakabuku & Josephat Kimaro

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Pauline Philipo Gekul (Mb) amefanya ziara na kuzungumza na Menejimenti  ya Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), tarehe 17 Machi, 2023.

Kupitia ziara hiyo, Mhe. Gekul amepokea taarifa ya utekelezaji pamoja na  kujengewa ufahamu kuhusu kazi na majukumu ya Wakala ya kuwahudumia Wananchi kutoka kwa Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi. Angela Anatory.

Mara baada ya kupokea taarifa hiyo, Mhe. Naibu Waziri ameipongeza RITA kwa mageuzi makubwa wanayofanya kwa kuwezesha wananchi kuweza kutuma maombi  ya huduma kidijitali popote walipo bila kufika katika ofisi za Wakala. Pia akaitaka RITA kuhakikishwa kwamba a mifumo ya utoaji huduma inayotengenezwa inakuwa rafiki ili kuwawezesha wananchi hata wasio kuwa na upeo mkubwa wa teknolojia kuweza kuitumia kwa urahisi kwani wapo wananchi ambao uelewa wao ni mdogo katika masuala ya matumizi ya mitandao.

Aidha, ameitaka RITA kushirikiana na wadau wengine kuimarisha usimamizi wa masuala ya Mirathi ili kupunguza migogoro inayozidi kuongezeka katika jamii huku wananchi wengi wakidhulumiwa haki zao. Mhe. Gekul pia akaagiza elimu kuhusu mirathi iongezwe ili wananchi waweze kuzitambua haki zao.

Kwa Mhe. Gekul, hii ni ziara yake ya kwanza kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria tangu kuteuliwa kwake na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mwezi Februari mwaka huu.