NALIS KULETA MAPINDUZI KATIKA URATIBU NA UPATIKANAJI WA HAKI NCHINI
Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha utoaji wa haki nchini kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa, huku ikikutanisha viongozi na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za mnyororo wa Haki Jinai kujadili maendeleo ya Mfumo wa National Legal Information System (NALIS).
Akifungua kikao hicho Juni 03, 2026 Mtumba Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki Bi. Jane Lyimo, akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. John Jingu alisema kuwa Wizara ya Katiba na Sheria ina jukumu la kuratibu, kusimamia na kufuatilia upatikanaji wa haki nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, kwa usawa na kwa ufanisi.
Alibainisha kuwa kutokana na matumizi ya TEHAMA upo umuhimu wa kuwa na mfumo wa pamoja wa ukusanyaji na usimamizi wa taarifa, hivyo Wizara imeanzisha Mfumo wa National Legal Information System (NALIS), unaolenga kuunganisha huduma mbalimbali za Wizara pamoja na taarifa kutoka taasisi za sekta ya haki ili kuongeza uwazi, uwajibikaji, uratibu na ufanisi katika utoaji wa haki nchini.
Bi. Lyimo alisema kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wa mnyororo wa Haki Jinai ili kujadili aina ya taarifa zinazohitajika kuingizwa katika mfumo huo, namna bora ya kuzipata pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi zinazohusika.
Aidha, alieleza kuwa NALIS itakuwa nyenzo muhimu katika kuunganisha taasisi za Haki Jinai na kuwezesha kubadilishana upatikanaji wa taarifa kwa wakati, jambo litakalosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuimarisha utendaji kwa kuongeza uwajibikaji katika utoaji wa haki.
Bi. Lyimo aliwataka washiriki kutumia kikao hicho kutoa maoni, ushauri na mapendekezo yatakayosaidia kuuboresha Mfumo wa NALIS na kupitia maendeleo ya mfumo huo pamoja na kujadili aina ya taarifa zinazotarajiwa kupatikana ndani yake kwa manufaa ya sekta nzima ya haki nchini.