Nataka Watumishi Wawajibikaji – Maswi

William Mabusi na Hyasinta Kissima – WyKS Dodoma
Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Chacha Maswi amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuwajibika katika majukumu yao ili kutimiza malengo ya Wizara na matarajio ya wananchi.
Bw. Maswi ameyasema hayo kwenye hafla ya kukabidhiana ofisi kati yake na Bi. Mary Makondo aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala mkoa wa Ruvuma, tarehe 30 Julai, 2024 ofisi za Wizara Mtumba, hafla iliyohudhuriwa na watumishi na Menejimenti ya Wizara.
“Nawaomba mambo makubwa mawili; kwanza, nahitaji utumishi uliotukuka, utumishi huo uambatane na ushirikiano bila majungu wala makundi. Pili, nahitaji watumishi wawajibikaji.” Alisema na kuongeza “Tumeomba kazi wenyewe na wengine tumetoka Ukuryani sasa tufanye kazi.”
Akiongelea kuhusu ushirikiano kati ya Menejimenti na watumishi wa chini yao amesema, “Watumishi walio chini yako ndiyo wanaokufanya uwe boss hivyo tuwathamini na kuwasaidia. Hawa wadogo ndiyo wanatufanya tuwe Viongozi, orodha ya malipo inayokuja kwangu ianze na wadogo ili tuwasaidie na kuwatia moyo.”
Aidha, Bw. Maswi amewataka Wakuu wa Idata na Vitengo kuwaacha watumishi walio chini yao kuonyeshe uwezo wao, “kama sisi tusingepewa nafasi ya kuonyesha uwezo wetu tusingeaminiwa na leo kuwa hapa, tuwaache nao wajulikane kama hutaki mtu aonekane wewe mwanga?”
Akiongea katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kufanya mabadiliko ya uongozi kwa mujibu wa Katiba, “mabadiliko ambayo ameyafanya Mhe. Rais tumeyapokea na tunawatakieni kila la heri kwenye majukumu yenu mapya.” Amesema huku akimtaja Bw. Maswi kuwa ni kiongozi wa mabadiliko chanya.
Mhe. Sagini amewasihi watumishi wa Wizara kuendeleza umoja, “ameondoka Mary amekuja Maswi, nasaha zangu kwenu nikitumia maneno ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Kikwete, nanukuu,"mimi Jakaya Kikwete nimemaliza muda wangu na sasa anakuja Rais ambaye approach yake ya mambo inaweza kuwa tofauti.” mwisho wa kunuu. Naomba mtambue Katibu Mkuu sasa ni Maswi, tujifunze kwa wapesi na kufanya anavyotaka, tuache kulinganisha Mary na Maswi.
Aidha, Mhe. Sagini amemshauri Katibu Mkuu huyo kuratibu vikao vya mara kwa mara na Wakuu wa Taasisi za Wizara ili kuepusha vikao vya dharura kwa lengo la kuongeza ushirikiano kati ya Taasisi za Wizara.
Akiongea katika hafla hiyo Bi. Makondo amempongeza Katibu Mkuu mpya kwa kuteuliwa kuwatumikia wananchi kupitia Wizara ya Katiba na Sheria. Wizara ambayo imepewa jukumu la kusimamia masuala ya haki na sheria huku akiwataka watumishi kumpa ushirikiano.