MFUMO NALIS KUIMARISHA UTOAJI WA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA NCHINI.
Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini, kupitia mafunzo ya Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Huduma za Kisheria (NaLIS), yaliyotolewa kwa Wasajili Wasaidizi wa Mikoa na Wanasheria wa Mikoa, kwa lengo la kuwawezesha kutumia mfumo huo kwa ufanisi katika kuwahudumia wananchi.
Mafunzo hayo yametolewa na Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara ya Katiba na Sheria, Gabriel Omary, wakati wa kufunga Kikao Kazi cha Wasajili Wasaidizi wa Mikoa na Wanasheria wa Mikoa kuhusu uendelevu na uimarishaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini, kilichofanyika tarehe 16 na 17 Septemba 2026 katika Ukumbi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Morogoro.
Katika mafunzo hayo, wajumbe walipatiwa uelewa na ujuzi kuhusu matumizi ya NaLIS katika kurahisisha ukusanyaji, uwasilishaji na usimamizi wa taarifa zinazohusu huduma za msaada wa kisheria, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuwezesha taarifa muhimu kupatikana kwa wakati.
Aidha Omary amesema matumizi sahihi ya mfumo huo yatawawezesha Wanasheria na Mawakili wanaotoa huduma za msaada wa kisheria kufuatilia na kusimamia kwa ufanisi huduma zinazotolewa kwa wananchi, pamoja na kuwezesha taarifa za huduma hizo kutumika katika kupanga na kuboresha utoaji wa msaada wa kisheria nchini.
Amesisitiza umuhimu wa kila mshiriki kutumia ujuzi walioupata katika mafunzo hayo katika maeneo yao ya kazi, ili NaLIS iwe chombo muhimu cha kuongeza ufanisi, uwazi na upatikanaji wa taarifa katika huduma za msaada wa kisheria, na hatimaye kuwawezesha wananchi kupata haki kwa wakati na kwa ufanisi.
Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Katiba na Sheria kutumia mifumo ya kidijitali kuimarisha huduma za upatikanaji haki nchini, ikiwa ni mchango katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga Taifa lenye haki, fursa na maendeleo jumuishi