Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Ndumbaro afungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Imewekwa: 19 Apr, 2023
Ndumbaro afungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Na Mwandishi wetu.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amefungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Takwimu Jijini Dodoma tarehe 18 Aprili, 2023.

Akifungua Mkutano huo wenye lengo la kuwapitisha watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Taarifa ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/24 ya Ofisi hiyo ambapo watumishi watapata wasaa wa kuchambua vipaumbele vya mpango na bajeti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mwaka 2023/24 ili kuhakisha mafanikio yaliyofikiwa mwaka 2022/2023 yanaongezeka.

Aidha, Mhe. Ndumbaro amewaasa watumishi wa Ofisi hiyo kuweka juhudi katika kutekeleza majukumu yao ili kulinda taswira ya jamii na kuwa chachu ya mabadiliko.

Vile vile Mhe. Ndumbaro ametoa rai kwa viongozi wa Baraza hilo kutumia Baraza hilo kama njia ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Baraza ambaye katika Hotuba yake aliwaasa watumishi wa Ofisi hiyo hususan Wakuu wa Divisheni na Vitengo waendelee kuwasilisha taarifa za utendaji kazi za kila wiki kwa kuainisha kazi zilizopokelewa, zilizotekelezwa na ambazo hazijatekelezwa kwa kuwa taarifa hizo zitasaidia kufanya tathmini kuhusu utendaji kazi.

Jaji Dkt. Feleshi amewasihi watumishi wote hususan watumishi wote ambapo wamepatiwa vifaa vya TEHAMA kuvitumia kwa uangalifu kwa malengo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya Ofisi na Serikali kwa ujumla.