Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Ndumbaro awataka Waandishi kuepuka kuwa sehemu ya ukatili wa kijinsia

Imewekwa: 14 Jul, 2023
Ndumbaro awataka Waandishi  kuepuka kuwa sehemu ya  ukatili wa kijinsia

Na Lusajo Mwakabuku - WKS 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewaasa Waandishi wa habari kutotumia taaluma yao katika kusambaza taarifa ambazo zinachochea ukatili wa kijinsia bali wasimamie misingi ya uandishi na utoaji wa taarifa wenye lengo la kuelimisha na kuhabarisha na hatimaye kukuza ustawi wa jamii.

Waziri Ndumbaro ameyasema hayo tarehe 14/07/2023 wakati akizindua mafunzo ya siku mbili kwa Wahariri na Waandishi wa Vyombo vya Habari mbalimbali ambao wapo kwenye timu ya kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia inayosimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria.

“Ndugu zangu Wanahabari, wakati wa kuripoti masuala ya ukatili wa kijinsia, kumbukeni mnafanya kazi hii kwa lengo la kutokomeza masuala haya, naomba niwasihi msimamie misingi ya uandishi na utoaji wa taarifa kwa umma ili isije kuwa taarifa zenu badala ya kuonesha ubaya ili kuzuia uendelezwaji wa matukio haya, zikachochea tena ukatili.” Alisema Ndumbaro.

Aidha, Ndumbaro aliwataka Wanahabari hao kujikita kwenye kutoa taarifa zenye mwendelezo wa ushughulikiwaji wa tukio husika kwa lengo la kusaidia wananchi kufahamu hatua zinazochukuliwa hadi kufikia haki ya muhusika. Ndumbaro pia akavitaja vyombo mbalimbali vinavyotumika kumsaidia manusura ikiwemo huduma za usaidizi wa kisheria, simu za dharura, malazi na vituo vya dharura vya hifadhi ya manusura wa ukatili wa kijinsia huku akiwataka Waandishi kuzipa umuhimu taarifa hizi katika kurasa za kwanza za machapisho ili kusaidia kujenga ufahamu na uelewa kwa wananchi kuhusu wapi pa kukimbilia kupata msaada kunapotokea changamoto za ukatili wa kijinsia.

Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi kutoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Msaada wa Kisheria Bi. Ester Msambazi alisema Wizara imekuwa ikishirikiana na Wadau mbalimbali katika kuhakikisha mwananchi anapata huduma za kisheria kwa urahisi na kwa gharama nafuu. "Moja ya wadau tunaofanya kazi nao kwa ukaribu ni tasnia ya Habari kwa kuwa wana mchango mkubwa sana katika kuwafikia wananchi kupitia vipindi vya redio, televisheni na hata njia nyingine wanazozitumia." 

“Hii ni awamu ya tatu mafunzo haya yakitolewa na kama Wizara tumeona mafanikio makubwa kwa washiriki kwani kupitia makundi ya WhatsApp washiriki wamekuwa wakituma kazi zao walizofanya na kurusha mijadala mbalimbali inayohusu vitendo vya ukatili wa kijinsia.” Alisema Bi. Msambazi.

Kwa upande wake Mhariri wa Gazeti la Mwananchi na Mwenyekiti wa timu hiyo ya Wanahabari dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia Bi. Lilian Timbuka, akitoa salaamu za shukrani baada ya hotuba ya Mgeni Rasmi, alisema matukio ya kufanyika kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku na kubainisha kuwa inawezakana elimu imewafikia wananchi na hivyo uelewa juu ya madhara yanayotokana na ukatili na kufahamu sehemu maalumu ya kutolea taarifa umeongezeka. Aidha, akaongeza kuwa hivi sasa Vyombo vya Habari vinatumika kikamilifu katika kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia akisisitiza kuwa sio kwamba matukio yameongezeka bali wananchi sasa wamepata uelewa juu ya vitendo hivyo na njia sahihi za kuchukua.