Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

NDUMBARO AZINDUA KITABU CHA MASUALA YA AJIRA NA SHERIA ZA KAZI

Imewekwa: 31 Jan, 2023
NDUMBARO AZINDUA KITABU CHA MASUALA YA AJIRA NA SHERIA ZA KAZI

Imewekwa: Thursday 26, January 2023

 

NDUMBARO AZINDUA KITABU CHA MASUALA YA AJIRA NA SHERIA ZA KAZI

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amezindua kitabu cha masuala ya ajira na sheria za kazi chenye kurasa zaidi ya Mia Tisa jijini Dar es salaam na kuwataka watanzania wengine kujikita katika kuandika vitabu hasa vyenye uchambuzi wa kisheria ambavyo vitawaongezea uelewa watanzania juu ya sheria zao na haki wanazostahili.

Waziri Ndumbaro ameyasema hayo usiku wa jana Tarehe 25/01/2023 alipoalikwa kama Mgeni Rasmi kuzindua kitabu hicho kilichoandikwa na Wakili Msomi bwana Ally Kileo na kuongeza kuwa kitabu hicho kimegusa kila eneo muhimu katika mazingira ya ajira yakiwemo masuala ya haki ya kunyonyesha na ni kwa kiasi gani sheria hiyo inatakelezwa katika nchi yetu.

“Hiki ni kitabu changu cha Tano sasa kukizindua lakini katika vitabu vyote vinavyohusiana na masuala ya sheria hapa nchini hiki ni kitabu cha kwanza ambacho nimekiona kinaunganisha moja kwa moja suala la ajira na haki ya mama kunyonyesha” Alisema Ndumbaro.

Aidha Waziri Ndumbaro alisema kitabu hiki kimegusa maeneo muhimu kama vile sheria za uwekezaji zinavyotekelezwa hapa nchini na kuongeza kuwa kabla mwekezaji hajaamua sehemu ya kuwekeza, moja ya vitu muhimu anavyoangalia ni sheria za ajira ili kuepusha mikwaruzano kati yake na Serikali, hivyo kitabu hiki kitarahisisha taratibu za masuala ya uwekezaji kwani kinaelezea na kufafanua masuala yote muhimu yanayohusiana na sheria hizo sehemu za kazi.

Wakielezea kwa nyakati tofauti mapitio ya kitabu hicho, Prof. Chris Peter Mahina alisema kitabu hicho kimelenga kumfanya mtanzania kupambania haki zake katika maeneo mbalimbali ya ajira huku Dkt. Dominucus Makukula akielezea namna vyombo vya Habari vinavyosaidia ama kuvuruga pale ambapo mahusiano ya ajira kati ya mwajiri na muajiriwa yanapoharibika.

Wakili Ally Kileo wakati akitoa hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi alisema kitabu chake chenye kurasa 941 na sura 20 kimemchukua Miaka Mitano kukikamilisha na kinapatikana kwa nakala ngumu (hard copy) na laini (softcopy).