Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

OFISI MPYA YA MASHTAKA SINGIDA KURAHISISHA HUDUMA  KWA WANANCHI

Imewekwa: 13 Mar, 2026
OFISI MPYA YA MASHTAKA SINGIDA KURAHISISHA HUDUMA  KWA WANANCHI

Wananchi  wa  Mkoa wa Singida wanatarajia kunufaika  na  huduma zinazotolewa  na  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa ofisi hizo utakaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 2.4 hadi kukamilika kwake. 

Hayo yamebainishwa mkoani Singida,13 Machi, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakati ambapo kamati hiyo ilitembelea, kukagua na kupokea taarifa ya maendeleo ya mradi wa ujenzi wa ofisi hizo unaotekelezwa na Serikali kupitia  bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026. 

Katika ziara hiyo, wajumbe wa Kamati hiyo walipokea taarifa ya  maendeleo ya ujenzi na kupata fursa ya kujionea hatua mbalimbali za ujenzi wa jengo  hilo la ofisi  ambao unatarajiwa kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za mashtaka na haki kwa wananchi plae litakapokamilika. 

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo Mwenyekiti  wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Ndumbaro ametoa pongezi kwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha sekta ya haki nchini kupitia uwekezaji katika miundombinu ya taasisi za  Sheria ambapo mpaka sasa  Serikali tayari imekamilisha taratibu za malipo yanayohitajika na  Mkandarasi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika  kwa wakati uliopangwa bila kuwa na mkwamo wa kifedha. 

Aidha, Mhe. Dkt. Ndumbaro alimtaka Mkandarasi kuongeza juhudi katika utekelezaji wa kazi ili ukamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma muhimu za Mashtaka kwa wananchi wa Singida na maeneo jirani. 

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Mhe. Halima Dendegu, amekiri wazi kuwa  uwepo wa ofisi hiyo pindi ujenzi utakapokamilika ni dhamira ya wazi ya kuhakikisha uhalifu unashughulikiwa kwa mujibu  wa Sheria na haki inapatikana kwa Wananchi. 

Mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Singida ulianza tarehe 10 Machi 2025 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2026, ambapo 
kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kisheria na kuimarisha upatikanaji wa haki  kwa wananchi