Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

KAMATI YA BUNGE YAJADILI UENDESHAJI WA MASHAURI YA MAKUNDI MAALUM

Imewekwa: 19 Aug, 2026
KAMATI YA BUNGE YAJADILI UENDESHAJI WA MASHAURI YA MAKUNDI MAALUM

Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha upatikanaji wa haki kwa mashauri ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu katika vyombo vya upatikanaji haki nchini
 
Hayo yamesemwa Agosti 18,2026 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera wakati akiwasilisha taarifa kuhusu uendeshaji wa mashauri ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu katika vyombo vya upatikanaji haki nchini mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.
 
Dkt. Homera amesema miongoni mwa hatua hizo ni pamoja  na Mahakama ya Tanzania kutunga Kanuni za Sheria ya Mahakama na Matumizi ya Sheria (Mwenendo na Taratibu katika Mashauri Yanayohusu Makundi yaliyo katika Mazingira Hatarishi), 2019, zinazoweka utaratibu maalum wa uendeshaji wa mashauri hayo.
 
Aidha Dkt.Homera amesema kanuni hizo zinalenga kuharakisha uamuzi wa mashauri, huku zikiweka muda wa uendeshaji wa mashauri hayo kuwa miezi minne  tangu shauri linaposajiliwa Mahakamani. 
 
Pia, Dkt.Homera amesema Serikali imeanzisha Jukwaa la Kitaifa la Haki Mwanamke mwaka 2023 kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa haki, ulinzi na uwezeshaji wa wanawake nchini.
 
Kwa upande wao, wajumbe wa Kamati wamepongeza juhudi za Mahakama katika kuboresha huduma za utoaji haki, pamoja na huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa kwa makundi mbalimbali, ikiwemo wanawake.
 
Awali akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, amesema upatikanaji wa haki ni suala la msingi kwa kila mwananchi bila kujali hali au mazingira yake, kwa mujibu wa Katiba.