TANZANIA YAELEZA MIKAKATI YAKE KATIKA KUPAMBANA NA UHALIFU WA KUPANGWA UNAOVUKA MIPAKA
Serikali ya Tanzania imetunga na kufanya maboresho ya sheria mbalimbali sambamba na mabadiliko ya kisera, ili kuimarisha udhibiti wa uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka na kufanikisha utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Hayo yamebainishwa Oktoba 19,2026 na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, mjini Vienna, Austria, ambapo alimuwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria katika Kikao cha 13 cha Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Uhalifu wa Kupangwa Unaovuka Mipaka (Conference of the Parties to the United Nations Convention against Transnational Organized Crime).
Mhe. Katimba amesema kuwa, kati ya jitihada zilizochukuliwa na Tanzania ni pamoja na kuimarisha taasisi zinazosimamia utekelezaji wa Mkataba huo, ambazo ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) , Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB).
Hatua hiyo imechangia mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya uhalifu huo, ikisaidiwa na ushirikiano wa karibu na mashirika ya kikanda na kimataifa kama vile INTERPOL, UNODC, SADC, na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumzia mapendekezo ya maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wa Mkataba yaliyotolewa na Tanzania katika kikao hicho, Mhe. Katimba ameyataja kuwa ni pamoja na ushirikiano wa kisheria na urejeshaji wa wahalifu au watuhumiwa (Mutual Legal Assistance and Extradition) , uchunguzi wa kifedha na urejeshaji wa mali zinazotokana na uhalifu ,usaidizi wa kitaalamu na kujenga uwezo wa kiutendaji.
Kikao hicho cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Uhalifu wa Kupangwa Unaovuka Mipaka kinafanyika kila baada ya miaka miwili, ambapo Tanzania ikiwa nchi mwanachama imepata fursa ya kuwasilisha ripoti na hatua inazochukua katika utekelezaji wake.