Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Patieni ufumbuzi masuala ambayo ni kero kwa wananchi: Dkt. Mpango

Imewekwa: 22 Jul, 2023
Patieni ufumbuzi masuala ambayo ni kero kwa wananchi: Dkt. Mpango

Na William Mabusi & George Mwakyembe – WKS Songea

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewataka wataalamu wanaotekeleza Kampeni ya Kitaifa ya msaada wa kisheria ijulikanayo kama Mama Samia Legal Aid Campaign kuyapatia ufumbuzi masuala wanayokutana nayo na kuonekana kuwa kero kwa wananchi wakati wa utekelezaji wa kampeni hiyo tangu ilipoanza Aprili mwaka huu ili watanzania wapate haki kwa wakati.

Mhe. Mpango ameyasema hayo wakati akizindua utekelezaji wa kampeni hiyo mkoani Ruvuma tarehe 22 Julai, 2023 mjini Songea.

“Fanyeni uchambuzi wa kina wa masuala mnayokutana nayo katika utekelezaji wa kampeni tangu ilipoanza kutekelezwa na kuyawekea mkakati wa kuyapatia ufumbuzi na kuweni tayari kuyabadili yale yatakayoonekana kuwa kero kwa wananchi ili haki ipatikane kwa wakati.” Alisema Dkt. Mpango.

Ameyataja baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa na changamoto na kuleta migogoro mingi kwa wananchi kuwa ni pamoja na migogoro ya umiliki wa ardhi, migogoro ya wakulima na wafugaji, kesi za madai ya mirathi, ukatili wa kijinsia na migogoro ya kazi na ajira.

Aidha, kuhusu utekelezaji wa hukumu za Mahakama ambapo mwananchi aliyeshinda kesi mahakamani anabaki na hukumu yake mikononi bila kupata haki yake, Makamu wa Rais amesema kampeni hiyo itoe elimu ya kutosha kuhusu taratibu za kufuata wakati wa  kutekeleza hukumu za Mahakama ili mwananchi apate haki na isiwe haki ambayo imeishia kwenye makaratasi.

Kwenye eneo hilo hilo la elimu Dkt. Mpango amesema itolewe elimu kuhusu upatikanaji wa haki kwa walemavu “Kampeni hii itoe elimu kuhusu upatikanaji wa haki kwa watu wenye ulemavu. Kwa mujibu wa Katiba watu wote ni sawa mbele ya sheria hivyo watu wenye ulemavu walindwe na kupata haki kama watu wengine.”

Aidha, amewataka wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria kutumia fursa hiyo kikamilifu na amewasihi wananchi wote kuendelea kutekeleza wajibu wao katika malezi ya watoto, ulinzi wa haki za makundi maalumu, kutoa taarifa juu ya vitendo vya kiuhalifu na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya haki pindi wanapohitajika. 

Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Songea Mjini Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema Kampeni hiyo inayotekelezwa kwenye mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar imeshafanyika Mikoa ya Dodoma, Manyara, Shinyanga na sasa Mkoa wa Ruvuma.

Katika mikoa hiyo mitatu Halmashauri 21, Kata 210, Vijiji 525 zimepitiwa ambapo migogoro ya kisheria 2,325 imetatuliwa hali inayopelekea kuleta amani kwenye jamii, ambayo ndilo lengo kuu la kampeni kama ambavyo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akiagiza.

Mhe. Ndumbaro amezishukuru Asasi za Kiraia, Mashirika yanayotoa msaada wa sheria TANLAP na LSF, Chama cha Mawakili Tanganyika, Benki ya NMB na Wadau wa Maendeleo kwa michango yao katika utekelezaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign.

Pia amevishukuru Vyombo vya Habari kwa kuibua changamoto mbalimbali kwenye jamii, kufikisha elimu kwa wananchi, kupambana na ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia, mila potofu na kusaidia kuainisha maeneo yenye migogoro kwenye jamii.