Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Pelekeni kwa Wananchi Elimu ya Sheria Mliyopata: Dkt. Kazungu

Imewekwa: 14 Oct, 2023
Pelekeni kwa Wananchi Elimu ya Sheria Mliyopata: Dkt. Kazungu

Na William Mabusi – WKS Morogoro

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu ametoa rai kwa washiriki wa mafunzo ya Sheria ya Ulinzi wa Watoa Taarifa na Mashahidi ya mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2023 kupeleka elimu waliyoipata kwa wananchi ili watambue jitihada zinazofanywa na Serikali za kuendelea kupambana na uhalifu nchini.

Dkt. Kazungu ametoa rai kwenye hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Bw. Burton Mwasomola Mkurugenzi Msaidizi wa Katiba wakati wa kufunga mafunzo ya Sheria ya Ulinzi wa Watoa Taarifa na Mashahidi ya mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2023 kwa Maafisa Waandamizi Wachunguzi kutoka Taasisi Chunguzi na Waendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, tarehe 13 Oktoba, 2023 Mkoani Morogoro.

“Rai yangu mkaendelee kutoa elimu kwa umma wa watanzania na watumishi wenzenu kuhusiana na malengo ya Sheria hii na Kanuni zake ili wafahamu umuhimu wa kuwafichua wahalifu wa makosa mbalimbali ili hatimaye kutokomeza mtandao wa uhalifu nchini,” alisema.

Dkt. Kazungu aliongeza kuwa, “katika kutekeleza majukumu yenu mna watu ambao huwatumia kuwapa taarifa za uhalifu, kupitia mafunzo haya kawaambieni kwamba Serikali imeweka utaratibu wa ulinzi kwao pale ambapo itaonekana maisha yao yako hatarini kutokana na taarifa za uhalifu watakazotoa.”

Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wengine, aliyekuwa Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Wakili wa Serikali Bi. Florida Wenceslaus amesema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa wa Sheria ya Ulinzi wa Watoa Taarifa na Mashahidi ya mwaka, 2015 na Kanuni zake za mwaka 2023 na hivyo kwenda kurahisisha utendaji kazi wao kwani utekelezaji wa Sheria hiyo utawapa hamasa wananchi kutoa taarifa za uhalifu.