Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Rais TLS Aishauri Wizara Kujikita Kwenye Mageuzi ya Haki Jinai

Imewekwa: 29 Jun, 2024
Rais TLS Aishauri Wizara Kujikita Kwenye Mageuzi ya Haki Jinai

William Mabusi – WKS Morogoro

Mtaalam Mshauri wa mradi wa Programu ya Kujenga Uwezo wa Taasisi katika Kupambana na Rushwa Nchini – BSAAT na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Harlod Sungusia ameishauri Wizara ya Katiba na Sheria kujikita kwenye mageuzi ya haki jinai ili kuwaongezea imani wananchi kwenye mifumo ya haki jinai na namna ya kushughulika na uhalifu wa kifedha.

Wakili Sungusia ameyasema hayo alipokuwa anatoa mada ya Utekelezaji wa Mradi wa BSAAT na Upimaji Matokeo ya Mradi huo na Mpango Kazi kwa mwaka 2024/25. Juni 29, 2024 mjini Morogoro.

“Mradi wetu wa BSAAT unafika ukomo mwezi Machi, 2025. Nashauri baada ya ukomo wa BSAAT Wizara kujikita kwenye mageuzi ya haki jinai na namna ya kushughulika na uhalifu wa kifedha yaani utakatishaji fedha haramu na makosa tangulizi katika utakatishaji fedha haramu.” Alisema.

Wizara ya Katiba na Sheria inaendesha Vikao Kazi viwili mkoani Morogoro; cha kwanza kikiwa na jukumu la kufanya tathmini ya mradi huo kwa kazi zilizofanywa mwaka 2023/24 na kuandaa Mpango Kazi wa mradi kwa mwaka 2024/25, Kikao Kazi cha pili kinaandaa Andiko la Kuanzisha Mfuko wa Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi.