Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Sagini Afurahishwa na Mapokezi MoCLA

Imewekwa: 08 Apr, 2024
Sagini Afurahishwa na Mapokezi MoCLA

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Naibu Waziri mpya wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amestushwa na mapokezi makubwa yaliyofanywa na Viongozi wa Wizara hiyo pamoja na Watumishi na kukiri kuwa hiyo ni mara yake ya kwanza kukutana na mapokezi makubwa kiasi hicho.

Mhe. Sagini ameyasema hayo wakati akiongea na Watumishi wa Wizara hiyo alipopokelewa kwa mara ya kwanza Wizarani hapo tarehe 8 Aprili, 2024 baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo.

“Haya ni mapokezi ambayo nilikowahi kupita sijawahi kukutana nayo, lakini Wizara ya Katiba na Sheria mko vizuri sana, napokea mapokezo hayo kama ishara ya mahusiano mema, ambacho ni kitu kizuri kwenye utumishi wa umma katika kufikia malengo ya taasisi.”

Mhe. Sagini amesisitiza upendo mahala pa kazi huku akionya kwamba kufanya kazi kwa upendo haina maana kumezea yale mabaya “tukifanya kazi kwa upendo matokeo yatakuwa mazuri sana, upendo kwa wenzetu haina maana kumezea ya hovyo, kuchukua hatua dhidi ya maovu pia ni upendo. Ili kuleta mwenendo mzuri unaotakiwa, wanao tenda mema lazima waone waliofanya vibaya wanakemewa, wanaelekezwa kubadilika au wanachukuliwa hatua stahiki kulingana na matendo yao vinginevyo hakuna maana ya anayetenda mema aendelee kutenda mema.”

Katika kuielewa Wizara hiyo inavyofanya kazi amesema “nitajifunza kwa kasi kazi za Wizara ili kutimiza matarajio ya Waziri Pinda, matarajio ya watumishi lakini pia kutimiza matarajio ya Mhe. Rais na Watanzania kwa ujumla.” Aidha, amewataka Watumishi na Viongozi wenzake kumpa ushirikiano ili dhamira ya Rais ya kumpeleka Wizarani hapo iweze kuzaa matunda.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema yeye na timu nzima ya watumishi wa Wizara wanamtakia majukumu mema na kwamba wako tayari kufanya kazi naye ili kutoa matokeo nyanya kwenda na kasi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Baada ya mapokezi hayo watumishi na Viongozi wa Wizara walijumuika kwenye iftar iliyoandaliwa na Waziri wa Katiba na Seria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana na Katibu wa Wizara hiyo Bi. Mary Makondo, ikiwa ni Sadaka ya kuwafuturisha Watumishi, Wana Dododma na wageni mbalimbali walioalikwa.

Iftar hiyo iliambatana na dua ya kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mawaziri na Viongozi Waandamizi wa Serikali.

Akiongea katika iftar hiyo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mustafa Rajabu Shabani amesema “Kipindi hiki Viongozi wameutendea haki Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuanzia kwa mhe. Rais mwenyewe, Mawaziri na Viongozi mbalimbali wa Serikali ndiyo maana nchi yetu ina amani na utulivu ikiwa na majibu ya Mungu kwa matendo mema ya Viongozi wanayofanya katika nchi yetu.”