Sagini Aipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama na Kuitaka Kuzijengea Uwezo Kamati za Maadili
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini (Mb), ameipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuendelea kusimamia kwa weledi ajira na nidhamu za Watumishi wa Mahakama jambo ambalo limeongeza imani kubwa kwa Wananchi kwa Mahakama katika kusimamia utoaji Haki Nchini.
Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo Septemba 23, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye kikao na Watumishi wa Tume hiyo ambapo Watumishi hao wameongozwa na Katibu wa Tume Prof. Elisante Ole Gabriel na Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bi. Alesia Mbuya.
Mhe. Sagini amesema kuwa licha ya kuwepo kwa kazi kubwa inayofanywa na Tume zipo Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama katika ngazi ya Mikoa na Wilaya lakini Kamati hizo zimekuwa hazikutani kujadili majukumu ya msingi licha ya kuwa vikao hivyo vipo kwa mujibu wa Sheria.
"Kumekuwa na changamoto ya uelewa na Bajeti kwa Kamati hizi kushindwa kutekeleza majukumu yao. Ni vyema katika maandalizi ya bajeti tuone ni kwa namna gani Wizara zinaweza kuwasiliana na bajeti hizo zikahusishwa katika mwongozo wa bajeti kwa ajili ya kuzihudumia Kamati hizi." Alisema.
"Nitoe pongezi kwa Tume kwa kuendelea kuzitembelea na kuzijengea uwezo Kamati hizi za Mikoa na Wilaya ili ziweze kutambua majukumu waliyonayo na pia tuendelee kutoa elimu kwa jamii kuhusu uwepo wa Kamati hizi ili waweze kutambua umuhimu na majukumu ya Kamati katika kusimamia mnyororo wa Haki." Alisema Sagini.
Aidha, Naibu Waziri amesema Serikali ya Awamu ya sita imeendelea kuonesha dhamira ya dhati na umuhimu wa Tume hiyo ambapo kwa kipindi cha miaka minne kuongeza bajeti kutoka Bilioni 2.6 mpaka kufikia bilioni 5.5 mwaka 2024 ambapo inaonesha dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuiwezesha Tume katika kutekeleza majukumu yake.
Awali Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa kwa sasa Tume imejipanga kuendeleza matumizi ya mifumo katika masuala ya nidhamu na maadili, lengo ikiwa ni kuhakikisha Kamati za Maadili za Wilaya na Mikoa ziweze kutumia mifumo kujaza taarifa mbalimbali na kutunza kumbukumbu ili kupunguza muda na gharama za Naibu Katibu wa Maadili kufanya ufuatiliaji.