Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Sagini Aitaka Tume ya Haki za Binadamu Kutoa Elimu Juu ya Haki ya Kujieleza

Imewekwa: 10 May, 2024
Sagini Aitaka Tume ya Haki za Binadamu Kutoa Elimu Juu ya Haki ya Kujieleza

Na Yasinta Kissima – WKS Dodoma

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameitaka Tume ya Haki za Binadamu  na Utawala Bora kujipambanua katika majukumu yao na kutambua kazi inayofanywa na Serikali katika kutetea Haki za Binadamu na kuangazia baadhi ya watu wanaovuruga na kukashifu haki za wengine wakiwemo Viongozi  kwa sababu ya uwepo wa uhuru wa kujieleza.

Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo Mei 8, 2024 katika Makao Makuu ya Tume maeneo ya Kilimani jijini Dodoma ikiwa ni mwanzo wa ziara yake  ya kuzitembelea Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo kwa lengo la kujifunza na kufahamu majukumu yao katika kufanikisha kazi za Wizara.

"Jukumu la Tume ni kuangalia kwa kiwango gani haki za Binadamu na Utawala Bora zinatekelezwa na Taasisi mbalimbali za Umma au hata watu binafsi katika majukumu yao. Yapo mambo mengi ambayo Serikali imefanya yanayogusa haki za Binadamu lakini je katika ripoti zinazoandikwa na Tume hayo yameripotiwa?" Alihoji Mhe. Sagini

Aliendelea kusema, "Serikali ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya maamuzi magumu kufanya elimu ya msingi kuwa miaka kumi, utoaji wa elimu bila malipo mpaka kidato cha sita, ujenzi wa Zahanati na Hospitali katika maeneo mbalimbali. Kwenye Demokrasia imetoa uhuru wa  watu kutekeleza majukumu yao ya kisiasa yote haya yanalenga  kulinda Haki za Binadamu. Lakini wanaibuka watu na lugha za kejeli, lugha za matusi na lugha za kufedhehesha Viongozi wetu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iangalie na kujitokeza hadharani kuelimisha watu juu ya yale wanayoyaona  na yale yanayotendwa na Watanzania." Alisema Naibu Waziri.

Aidha, Sagini ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuboresha mahusiano na ushirikiano mahali pa kazi ili kuleta mafanikio na ufanisi  katika kutimiza malengo ya Taasisi.