Sagini Akoshwa Na Ubunifu wa Mahakama Katika Kuwatumikia Wananchi

Hyasinta Kissima, WyKS Dodoma
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini Julai 11, 2024 jijini Dodoma, amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel, ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kuzitembelea na kujifunza majukumu ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Katika mazungumzo hayo yaliyotanguliwa na kulitembelea jengo la Makao Makuu ya Mahakama yaliyopo Tambukareli jijini Dodoma, Naibu Waziri amefurahishwa na maboresho makubwa yaliyofanywa na Mhimili wa Mahakama ikiwemo ujenzi wa jengo la Mahakama lenye Teknolojia na vifaa vya kisasa ambalo litakuwa miongoni mwa majengo makubwa sita bora Duniani lenye thamani ya Shilingi Bilioni 129.7 fedha kutoka mapato ya ndani ya Serikali.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa, maboresho yanayofanywa katika Mhimili wa Mahakama kama vile upatikanaji wa vifaa vya kisasa, rasilimali watu, ujenzi wa miundombinu ya kisasa, matumizi ya TEHAMA, yameleta mchango mkubwa katika ubora wa utoaji haki Nchi na imani ya Wananchi kwa Mahakama imeongezeka maradufu.
"Nilipopewa jukumu la kumsaidia Mhe. Waziri Dkt. Balozi Pindi Chana katika Wizara ya Katiba na Sheria, nilisema lazima nijue hiki ninachoenda kukifanya.Tunapokea ripoti mbalimbali na tunazisoma. Lakini, ningeishia kwenye ripoti pekee bila kufika katika jengo hili na nimetembelea jengo hili sura ni tofauti kabisa.” Alisema Sagini.
Aliendelea kusema, "Nimeona makubwa kwenye TEHAMA. Jaji Mkuu aliniambia uje utembelee kwa kweli mna maajabu. Ninaweza kuona taarifa ya Mahakama ya Mkoa fulani, inafanya nini, shauri gani limepangwa kusikilizwa, mashahidi au hukumu inatolewa kwamba hiyo taarifa ninaweza kuipata hapa. Lakini malalamiko ya Wananchi kituo cha huduma kwa mteja kwamba kutakuwa na watu masaa 24 kusikiliza kero za Wananchi, na kuzitafutia masuluhisho, huu ni ubunifu mkubwa sana. Niwapongeze Mahakama kwa dhati ya moyo wangu kuwa mmefanya ubunifu katika kuwatumikia Wananchi."
Naibu Waziri Sagini amemshukuru Rais wa wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuja na wazo la ujenzi wa jengo la Mahakama 2012, kutambua jitihada za Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuanza ujenzi 2020 na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan 2021 kuendeleza ujenzi kwa kasi na kukubali kotoa fedha zote mpaka kufikia hatua hiyo.
Naibu Waziri Sagini amesema kuwa, Wizara ya Katiba na Sheria inaimani na kazi kubwa inayofanywa na Mahakama na itaendelea kushirikiana nao na kuisemea Mahakama katika majukwaa mbalimbali na pia kuitumia Mahakama kupitia maboresho yaliyofanyika kuwa sehemu ya eneo la kujifunza kwa Taasisi mbalimbali zilizopo chini ya Wizara na zinazohusika katika utoaji wa Haki kwa Wananchi.