Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Serikali ina Dhamira ya Dhati ya Kuanzishwa kwa Mradi wa Liganga na Mchuchuma – Waziri Chana

Imewekwa: 06 Jan, 2024
Serikali ina Dhamira ya Dhati ya Kuanzishwa kwa Mradi wa Liganga na Mchuchuma – Waziri Chana

Na Lusajo Mwakabuku – WKS Njombe

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha mradi huu unatekelezwa mapema iwezekanavyo ndio maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha malipo ya fidia kwa wananchi wote waliopisha eneo la utekelezaji wa mradi mkubwa wa Liganga na Mchuchuma Wilayani Ludewa Mkoani Njombe.

Waziri Chana ameyasema hayo tarehe 05/01/2023 akiwa katika Kijiji cha Nkomang’ombe kilichopo katika wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani humo akitekeleza jukumu lake la kusimamia misingi iliyowekwa na Sheria Sura 449 na 450 yenye lengo la kuhakikisha uwekezaji katika uvunaji na matumizi ya utajiri asili na maliasilia za nchi unatekelezwa kwa namna ambayo inainua hali ya wananchi kiuchumi na kuongeza pato la Taifa.

“Lengo la ziara hii ni kufuatilia utekelezaji wa Sheria hizi katika miradi ya Liganga na Mchuchuma. Aidha, Sheria hizi zinaweka misingi ya kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Ludewa na waliopo karibu na maeneo ya miradi hii wananufaika na fursa zinazopatikana katika uwekezaji wa rasilimali za Taifa. Kwa mfano, ni matarajio ya Serikali kuwa, uwekezaji wa miradi ya namna hii itatoa ajira kwa watanzania, itatoa fursa ya watanzania kusambaza zabuni kwa watanzania na kuwapa mafunzo yanayolenga kuhuisha teknolojia kwani kwa kufanya hivyo ndiyo utekelezaji wa misingi iliyowekwa na Sheria zetu.”alisema  Waziri Chana.

Aidha, Waziri Chana amesema kuwa pamoja na kwamba mradi huo una historia ndefu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha nia ya wazi ya kutekeleza mradi huo kwa kutoa kiasi hicho cha fedha ili miradi hiyo inaojumuisha uchimbaji wa chuma Liganga pamoja na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma ianze kazi mara moja baada ya maafikiano ya kimikataba kufikiwa.

Waziri Chana pia akatumia nafasi ya ziara yake ya siku mbili kuongea na wananchi wa vijiji vya Nkomang’ombe na Mundindi ambapo miradi hiyo inatekelezwa na kuwataka wawaandae vijana wao katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kielimu, uwekezaji mdogo mdogo na ujuzi ili mradi utapoanza basi waitumie nafasi hiyo vizuri kuhakikisha wanufaika wa kwanza wanakuwa wananchi wa maeneo husika.

Akiongelea hatua mbalimbali za kitaalam ambazo mradi huo umepitia, Meneja wa Mradi wa Liganga na Mchuchuma kutoka NDC Dkt. Witness Ishuza alisema “Mwaka 2013 Tafiti ya Makaa za mawe pamoja na Chuma zilifanyika, kwa kipindi hicho na  kugundua kwamba kuna tani milioni 428 za Makaa ya mawe katika eneo la ukubwa wa mraba 30 ambazo zinaweza kuchimbwa kwa miaka zaidi ya 140  na Chuma ambacho ni zaidi ya tani milioni 126 ambacho kinaweza kuchimbwa kwa miaka 58.”

Naye Mwenyekiti wa CCM katika Wilaya ya Ludewa amesema Rais Samia amefanya jambo kubwa kwani ametekeleza jambo ambalo ni kiu kubwa ya wananchi na kwamba Taifa litakwenda kusonga mbele kwani mradi huo unakwenda kubadilisha uchumi wa Taifa letu na kupunguza gharama kubwa zinazotumika katika kuagiza chuma kutoka nje tena kwa kutumia fedha za kigeni, hivi viwanda vyote vya nondo, viwanda vya umeme, viwanda vya mabati, vitatumia chuma chetu.

Rafael Memba mmoja wa wanufaika wa fidia ya kupisha mradi wa Liganga na Mchuchuma na mkazi wa Kijiji cha Nkomang’ombe alimshukuru Mhe. Rais Samia kwa kutimiza ahadi yake ya kulipa fidia licha ya kusubiri muda mrefu na pia akaiomba Serikali kuhakikisha taratibu mbalimbali zinazokwamisha mradi huo kuanza zinakalika kwa haraka ili mradi uweze kufanyika kwa haraka na kuleta mafanikio kwao binafsi na kwa Taifa kwa ujumla.