Serikali Kuendelea Kukisaidia Chama cha Msalaba Mwekundu
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dotto Biteko na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana wamesema Serikali itaendelea kukiwezesha Chama cha Msalaba Mwekundu nchini kutoa huduma za uokozi kwa wananchi wanaopatwa na madhira ama changamoto mbalimbali zinazoathiri maisha yao.
Kauli hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti wakati viongozi hao wakihutubia kwenye kilele cha Maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Mei 11, 2024 Jijini Dodoma.
Maadhimisho hayo yamefanyika Kitaifa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete na kuhudhuriwa na mamia ya wanachama wa Taasisi hiyo kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar yakibeba kauli mbiu isemaya “Natoa kwa furaha na furaha ninayotoa ni zawadi.”
“Ninyi huwa mstari wa mbele na kuhatarisha uhai wenu kwa kuokoa maisha ya watu wengine, kwa kufanya hivyo mnaisaidia Serikali katika utoaji wa huduma za kibinadamu kwa wahanga wa majanga mbalimbali, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Red Cross katika mazingira yote hata ya furaha.” Amesema Dkt. Biteko huku akimtaka Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Mhe. David Kihenzile kuendelea kuwasajili vijana kuongeza wanachama kwenye Chama hicho.
Naye Dkt. Chana akiongea kwenye maadhimisho hayo amesema ”Wizara itaendelea kuweka kanuni na miongozo mbalimbali kuhakikisha Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kinatimiza majukumu yake nchini. Aidha, Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Red Cross kuhakikisha Wananchi wanaopatwa na madhira na changamoto mbalimbali zinazoathiri maisha yao wanahudumiwa kwa wakati.”
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini na Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile amesema kwa sasa Red Cross ina Matawi 1600 Tanzania Bara na Zanzibar ikiwa na wanachama zaidi ya laki 6. Aidha, aliongeza kuwa Red Cross imo mbioni kujenga ofisi mpya kwenye mikoa 12 na kwamba ina mpango wa kujenga nyumba 35 kwa Watanzania waliobomolewa nyumba zao Wilayani Hanang’.
Katika Maadhimisho hayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye Kikatiba ndiye Mlezi wa Jumuiya hiyo ambaye aliwakilishwa na Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Dotto Biteko alitunikiwa Tuzo Maalum ya Ubinadamu ikiwa ni tuzo ya pili kutolewa hapa nchini, Tuzo kama hiyo iliwahi kutolewa kwa Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Nyerere.