Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

SERIKALI KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSI NA USAFIRISHAJI  HARAMU WA BINADAMU

Imewekwa: 23 Feb, 2026
SERIKALI KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSI NA USAFIRISHAJI  HARAMU WA BINADAMU

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ikiwemo utumikishwaji wa  kingono kwa watoto na usafirishaji haramu wa binadamu, kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata ulinzi na haki zao zinalindwa.

Akizungumza leo Februari 23, 2026 jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, amesema serikali itaendeleza juhudi hizo kupitia ushirikiano wa taasisi mbalimbali za haki jinai na wadau wa maendeleo.

Mhe. Katimba ametoa kauli hiyo alipotembelea Kikosi Kazi cha Ulinzi wa Mtoto dhidi ya Biashara ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu (AHTCP-TF), kwa lengo la kujionea namna kikosi hicho kinavyotekeleza majukumu yake ambapo amepongeza kazi inayofanywa na kikosi hicho kwa kushirikiana na wadau wengine katika kufichua na kuvunja mitandao ya kihalifu inayohusisha ukatili wa kingono kwa watoto.

“Hii kazi imeonyesha matokeo makubwa kwa mitandao ya usafirishaji haramu wa binadamu iliyokuwepo kukamatwa na kuwasaidia wahanga kurudi katika jamii zao,” amesema Mhe. Katimba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Divisheni ya Utaifishaji Mali na Makosa yanayovuka Mipaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) ambaye pia ni msimamizi wa Kikosi Kazi, Faraja Nchimbi, amesema kuwa kikosi hicho hakikuundwa kuchukua majukumu ya vyombo vya uchunguzi, bali kuunda timu ya wataalamu waliobobea katika masuala ya ulinzi wa mtoto.

Ameongeza kuwa kikosi hicho kinalenga kushughulikia mitandao mikubwa ya kihalifu inayojihusisha na usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na unyanyasaji wa kingono, kwa lengo la kung’oa mizizi ya uhalifu huo.

Naye Mkuu wa Kikosi Kazi hicho, SACP Tubalike Kasongwa, amesema kuwa katika operesheni mbalimbali zilizofanyika, manusura 233 wameokolewa na kupatiwa huduma za kisaikolojia, kiafya na kijamii ili kuwawezesha kurejea katika maisha yao ya kawaida.