SERIKALI KUIMARISHA MBINU ZA KUTATUA MIGOGORO YA NDOA KUPITIA USULUHISHI

Serikali imetambua haja ya kuimarisha mifumo ya kutatua migogoro ya ndoa kupitia usuluhishi, hususan kwa kuboresha utendaji wa bodi za usuluhishi wa migogoro ya ndoa kwa kuwajengea uwezo wasimamizi na wajumbe wake.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi ameyasema hayo jijini Arusha leo Septemba 29 20205 wakati akifungua kikao cha bodi za usuluhishi wa migogoro ya ndoa huku akiwakumbusha washiriki kuwa familia ndiyo msingi wa malezi, maadili na ustawi wa kijamii.
Maswi amesema migogoro na mivutano katika ndoa wakati mwingine husababisha talaka na katika baadhi ya matukio wazazi hupoteza maisha ya mmoja au wote wawili kutokana na migogoro hiyo huku wakiwaacha watoto wakihangaika na kuteseka na hivyo kuchangia ongezeko la watoto wengi wa mtaani.
"Takwimu za talaka kutoka kwa Msajili wa Ndoa zinaonesha kuwa mwaka 2021 kulikuwa na talaka 523, mwaka 2022 talaka 447, mwaka 2023 talaka 711, na mwaka 2024 talaka 1,569 zilisajiliwa," amesema Maswi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kwa Umma wa Wizara ya Katiba na Sheria, Angela Anatory amesema kuwa usuluhishi wa migogoro ya ndoa ni muhimu kwani husaidia wanandoa kuelewana na kuondoa uhasama baina yao.
"Usuluhishi hufundisha wanandoa kusikilizana na kuelewana vyema nyumbani; hupunguza lawama na chuki; na hata kama ndoa itavunjika, hakutakuwa na uhasama kati ya wanandoa waliotengana," amesema
Ameongeza kuwa Bodi imara za usuluhishi wa ndoa zitasaidia kupunguza tatizo la kuvunjika kwa ndoa nyingi na hivyo kuimarisha familia kwakuwa usuluhishi katika kushughulikia migogoro ya ndoa ni njia bora zaidi kuliko mapambano ya kisheria mahakamani, ambayo huacha majeraha na makovu ya kudumu.
Kwa upande wake, Profesa Cyriacus Binamungu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam alieleza kuwa kuna mapungufu katika utoaji wa huduma za usuluhishi kupitia Bodi za Usuluhishi wa Ndoa na Mabaraza ya Kata, kwani wakati mwingine hujigeuza kuwa mahakama kwa kutoa maamuzi badala ya kufanya usuluhishi.
Amesisitiza kuwa asilimia 99.9 ya wajibu wa bodi na mabaraza hayo ni kutoa usuluhishi, si maamuzi hivyo basi kitini cha mwongozo kitakapothibitishwa kitasaidia kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa wadau wanaohusika na usuluhishi wa migogoro ya ndoa nchini.