SERIKALI YAJIDHATITI KULETA MABADILIKO CHANYA KATIKA MNYORORO WA HAKI JINAI
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imedhamiria kupunguza changamoto ya ucheleweshaji wa mashauri, kuongeza ubora wa ushaidi pamoja na kuimarisha ufanisi wa mashauri ya jinai yanapofikishwa mahakamani ili kuongeza imani ya wananchi kwa vyombo vya dola na kudumisha amani, utulivu na utawala wa sheria nchini.
Haya yamesemwa jijini Dodoma leo tarehe 13 Aprili, 2026, na Mkurugenzi Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Jane Lyimo wakati akifungua rasmi mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Uchunguzi na Upelelezi kutoka katika taasisi mbalimbali za Haki Jinai nchini.
Bi Lyimo amesema, Wizara inaendelea kuimarisha uwezo wa Maafisa Uchunguzi na Upelelezi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki za binadamu na hivyo kuleta mabadiliko chants katika mnyororo wa haki jinai nchini.
“Mafunzo haya yanalenga kuwajengea uelewa mpana wa misingi ya kisheria katika uchunguzi wa makosa ya jinai, matumizi ya mbinu za kisasa na teknolojia katika upelelezi, kuboresha ukusanyaji, uhifadhi na uwasilishaji wa ushahidi pamoja na kusisitiza umuhimu wa uandishi sahihi wa jalada la kesi ili kuhakikisha ushahidi unaokusanywa unakua na uzito unaohitajika mahakamani” amesema Bi. Lyimo.
Aidha, Bi. Lyimo amesema kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Maafisa Uchunguzi na Upelelezi katika kuboresha mazingira ya kisheria na kiutendaji ili kuhakikisha kuwa mfumo wa Haki Jinai unakuwa imara, jumuishi na wenye kuaminika zaidi.
“Tutaendelea kuweka msukumo katika kuimarisha mifumo ya ulinzi wa Watoa taarifa/mashahidi ili kujenga imani kwa wananchi na kuhamasisha ushiriki wao katika mapambano dhidi ya uhalifu” alisisitiza Bi. Lyimo.
Mafunzo haya yanafanyika ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha mfumo wa Haki Jinai nchini pamoja na mchango wa Wizara katika kufikia DIRA 2050 inayolenga kuwa na Taifa lenye mfumo imara wa haki, unaoaminika na unaoweza kulinda haki za wananchi wote.