SERIKALI YASISITIZA: WAJUMBE WA BODI ZA USULUHISHI WA NDOA NI WASULUHISHI, SIO MAHAKIMU
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imezindua rasmi mafunzo ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Bodi za Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa kwa Mkoa wa Kagera ambapo pia imetoa maelekezo kwa wajumbe hao kuacha tabia ya kutoa hukumu badala ya kusuluhisha.
Akizungumza Mjini Bukoba leo, 8 Machi, 2026, wakati akifungua rasmi mafunzo hayo yanayowakutanisha Wajumbe kutoka Kata zote za Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Halmashauri ya Karagwe na Halmashauri ya Bukoba, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Franklin Rwezimula, amewataka wajumbe wa Bodi kujikita kutafuta suluhu zaidi kwa migogoro wanayoipokea badala ya kuhukumu.
"Wajumbe wa Bodi si Mahakimu, ninyi ni wasuluhishi, jukumu lenu si kutoa hukumu, bali kutumia kila njia zinazowezekana kusaidia na kuwezesha pande mbili kufikia muafaka," alisema Dkt. Rwezimula.
Aidha, Dkt. Rwezimula aliorodhesha changamoto zinazozikumba bodi hizo, ikiwemo ukosefu wa mafunzo ya kutosha kwa wajumbe wa Bodi, kutokuzingatiwa kwa taratibu sahihi za usuluhishi, ujazaji wa fomu usiozingatia Sheria, Bodi kutokujua mipaka yake, pamoja na wananchi kutokuwa na uelewa wa uwepo na umuhimu wa Bodi hizo.
Akitoa salamu za Mkoa na kumkaribisha Mgeni Rasmi, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Bw. Isaya Tendega alisema anaamini kwamba mafunzo haya yataleta mafanikio makubwa na kuziwezesha Bodi za Usuluhishi kuwa na uwezo zaidi wa kushughulikia changamoto za migogoro ya Ndoa. Alibainisha kwamba migogoro mingi ya Ndoa ambayo ingeweza kushughulikiwa vizuri na Bodi imekuwa ikifika kwa Wakuu wa Wilaya na mamlaka nyingine, hali inayoziongezea majukumu ambayo yangeweza kufanywa na Bodi kwa ufasaha zaidi.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria kwa Umma, Bw. Obadia Kameya, aliyetoa neno la utangulizi, alieleza kwamba mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa msingi wa Sheria ya Ndoa, Kifungu cha 102, Sura ya 29, kinachompa Waziri wa Katiba na Sheria mamlaka ya kuanzisha na kusimamia Bodi za Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa.
"Malengo ya mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wajumbe katika mbinu sahihi za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na kuzingatia maadili wakati wa usuluhishi," alisema Bw. Kameya,
Mafunzo haya si sehemu ya kutatua migogoro ya ndoa pekee bali pia ni daraja la kuimarisha taasisi ya familia ambayo ndio msingi wa jamii imara ikiwa ni utekelezaji halisi wa dira ya Uongozi wa Rais katika kujenga Taifa lenye mshikamano,maelewano na maendeleo endelevu.