Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

SHERIA YA UCHAGUZI INATOA FURSA YA KUFANYA UCHAGUZI HURU NA WA HAKI

Imewekwa: 21 May, 2025
SHERIA YA UCHAGUZI INATOA FURSA YA KUFANYA UCHAGUZI HURU NA WA HAKI

Wizara ya Katiba na Sheria imefanikiwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ikiwa ni miongoni mwa Sheria Kuu 57 kati ya Sheria Kuu 446 na Sheria ndogo 4,087 zilizotungwa na kufanyiwa marekebisho katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, wakati akielezea mafanikio ya Wizara ya Katiba na Sheria katika kipindi cha miaka minne cha Serikali ya Awamu ya sita, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro alisema kuwa Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 imefutwa baada ya kutungwa kwa Sheria mpya ya Uchaguzi, Sheria Namba Moja ya Uchaguzi ya Mwaka 2024.

Aliongeza kuwa sambamba na Sheria hiyo pia ipo Sheria pacha ambayo ni Sheria ya Tume ya Uchaguzi (Sheria Namba 2 ya Mwaka 2024) ambapo kwa mara ya kwanza kupitia Sheria hiyo Tume ya Uchaguzi inakuwa na Sheria yake kama Tume Huru.

“Wananchi waliomba mtu asipite bila kupingwa, viongozi wa chama wasisimamie Uchaguzi hivyo Sheria hii inataka nafasi za wasimamizi wa Uchaguzi zitangazwe, watu waombe na wafanyiwe usaili na watakaoshinda watapewa nafasi, waliomba pia wafungwa wapewe fursa ya kupiga kura na yote haya yamezingatiwa katika Sheria hii” alisema Dkt. Ndumbaro.

Aliongezea kuwa, Sheria hii inatoa uwanja mzuri wa kufanya Uchaguzi Huru na wa Haki na itaanza kutumika ifikapo tarehe 1 Julai, 2025 ambapo mabadiliko yoyote yanayoihusu Tume hii yatafuata taratibu zote za Kisheria.