SHERIA ZISIWE KIKWAZO KUFIKIA DIRA 2050: HOMERA
Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kufanyia maboresho Sheria mbalimbali ili kuendana na mahitaji ya maendeleo ya muda mrefu pamoja na kuziondoa Sheria zitakazo kuwa kikwazo katika kuvifikia vipaumbele vya Kitaifa ikiwemo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Juma Zuberi Homera, Jijini Dodoma leo 23 Machi,2026 wakati akifungua Kikao cha Nne cha Baraza la Nane la wafanyakazi wa Wizara na kusisitiza kuwa Sheria zinapaswa kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
“Ili kuifikia Dira 2050 tunapaswa kuwa na sheria imara na rafiki kwa maendeleo, bila maboresho hayo, tunaweza kuchelewa kuyafikia” alisema .
Aidha, Dkt. Homera ametoa wito kwa wajumbe wa Baraza hilo kuhakikisha kuwa mipango ya bajeti ya 2026/2027 inalenga kuleta ufanisi na matokeo chanya kwa Wizara na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndg. Eliakim Maswi, amesema kuwa pamoja na mwelekeo wa Bajeti ya 2026/2027 Baraza limelenga kuweka mikakati madhubuti katika kuhakikisha sekta ya Sheria inakuwa chachu ya maendeleo nchini.