Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Sheria zote kupatikana kwenye Mifumo ya kidijitali – Dkt. Ndumbaro.

Imewekwa: 14 Jul, 2023
Sheria zote kupatikana kwenye Mifumo ya kidijitali – Dkt. Ndumbaro.

Na George Mwakyembe - WKS

Waziri wa Katika na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameshuhudia utiaji saini wa mikataba miwili na Taasisi ya African Legal Information Institute (AfricanLII) ambayo imelenga kuhakikisha Sheria zote na maamuzi ya Mahakama vinapatikana kidijitali. Hayo yamefanyika tarehe 13 Julai 2023 jijini Dodoma. 

Mikataba hiyo imesainiwa kati ya AfricanLII na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na AfricanL II na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo na kufungua warsha ya upatikanaji endelevu wa kidijitali kwa sheria za Tanzania, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema mradi huo utahikikisha Sheria zote za Tanzania kubwa na Sheria ndogo zinapatikana kwenye mifumo ya kidijitali.

Dkt. Ndumbaro amesema “Hili haliishii kwenye sheria bali pia tunakwenda mpaka kwenye maamuzi ya Mahakama, falsafa ya Sheria inasema kutojua Sheria si utetezi. Hivyo Serikali imeamua kutekeleza kwa vitendo kwa kuhakikisha Sheria na maamuzi yanayotolewa na Mahakama zinapatikana kwa urahisi mahali popote pale kwa njia ya kidijitali.”

Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema hatua hiyo itasaidia kukuza upatikanaji wa haki kwa wananchi kirahisi zaidi lakini pia italeta ushirikiano na Taasisi na wadau wa Sheria wakiwemo wanaofanya tafiti pamoja na Walimu wa Vyuo Vikuu.

“Mradi huu pia utasaidia wananchi na taasisi za Serikali ambazo zinatumia sheria mbalimbali kuweza kuzipata kirahisi, ule muda wa kuondoka na kwenda maktaba ukatafute kitabu cha sheria uisome sasa umepitwa, tunatumia mapinduzi ya teknolojia kuhakikisha tunapeleka haki kirahisi na kwa wepesi kwa kila mtanzania,” alisema Dkt. Ndumbaro.

Vilevile Dkt. Ndumbaro amesema Serikali chini ya usimamizi wa Wizara ya Katiba na Sheria imekubali mfumo wa kidijitali kama mkakati wa kimsingi wa kurahisisha shughuli za Serikali, kuimarisha uwazi, na kuboresha utoaji wa huduma kwa umma, “Upatikanaji wa haki kwa Watanzania wote ni jambo la lazima katika Wizara ya Katiba na Sheria na miaka michache iliyopita, Wizara iliweka juhudi za ziada ili kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana nchini.”

Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema “tunafanya hivyo ili Sheria zetu zipatikane kwa urahisi na hii itawezesha watanzania hususan wanawake na wasichana kufikia huduma hiyo ili kudai haki zao na kutafuta suluhu.” Kwa kuona umuhimu wa hilo tayari Serikali imeanzisha Kampeni ya Mama Samia kutoa msaada wa kisheria ambayo tayari imefanyika kwenye mikoa ya Dodoma, Manyara na Shinyanga na kuwa wiki ijayo Kampeni hiyo itazinduliwa rasmi na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango katika Mkoa wa Ruvuma.

Dkt. Ndumbaro amesema pia Serikali imefikia uamuzi wa kutafsiri Sheria kwenda kwenye lugha ya Kiswahili ili zieleweke na watanzania wote na kuwataka wadau wanaotafsiri kuhakikisha wanatoa tafsiri zilizo sahihi.

Akiongea kwenye warsha hiyo mwakilishi wa GIZ Bw. Richard Shaba amesema hatua hiyo itasaidia kurahishia Serikali katika kutoa maamuzi na pia itaweka urahisi kwa watafiti wa Sheria na Walimu wa sheria.

Katika warsha hiyo viongozi mbalimbali wamehudhuria akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo.