Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

‘’SIKU 100 ZA RAIS SAMIA, MAGEUZI SEKTA YA SHERIA YALETA FURAHA KWA WANANCHI’’

Imewekwa: 15 Feb, 2026
‘’SIKU 100 ZA RAIS SAMIA, MAGEUZI SEKTA YA SHERIA YALETA FURAHA KWA WANANCHI’’

Na; Mwandishi wetu-Wizara ya Katiba na Sheria,

Katika siku 100 za mwanzo tangu kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 03 Novemba, 2025 Serikali kupitia wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kudhihirisha dhamira ya dhati ya kuimarisha misingi ya kuimarisha misingi ya haki, usawa na utawala wa sheria, kama nguzo kuu ya maendeleo ya Taifa.

Vipaumbele vya kitaifa Nchini Tanzania ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inatoa mwongozo katika sekta sheria kwa kusimamia utawala bora, haki, utawala wa sheria na misingi ya kikatiba ili kufikia adhma ya kujenga Taifa imara, jumuishi na lenye ustawi.

Kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, mafanikio makubwa yamepatikana katika kulinda maslahi ya Taifa, kuokoa fedha za umma, na kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi.

Siku mia moja katika Wizara ya Katiba na Sheria ni muda mfupi katika historia lakini imebeba maamuzi makubwa ushindi wa kisheria na mabadiliko yanayogusa Maisha ya Watanzania.

Haya ni mafanikio ndani ya siku 100 katika Wizara ya Katiba yanayoakisi dira ya Serikali ya kujenga Taifa lenye haki, usawa na uwajibikaji.

Serikali imekamilisha kutafsiri na kutangaza Sheria Kuu 433 kwa lugha ya Kiswahili, hatua inayowezesha wananchi kuelewa Sheria, kuimarisha uwazi, na kuimarisha utawala wa Sheria nchini. Hatua hii inalenga kuisogeza sheria karibu na wananchi kwa kuiondoa katika lugha ngumu ya kitaalamu na kuiweka katika Kiswahili kinachoeleweka.

Katika kuhakikisha wananchi wote, hususani wasiokuwa na uwezo wa kifedha, wanapata haki kwa usawa, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za msaada wa kisheria nchini. Wizara imeendelea kuimarisha uratibu wa huduma za msaada wa kisheria kupitia Kliniki za Msaada wa Kisheria zinazofanyika katika maeneo mbalimbali nchini. Kliniki hizo zilifanyika katika Mkoa wa Morogoro tarehe 5 na 6 Januari, 2026 na Mkoa wa Singida tarehe 9 hadi 10 Januari, 2026, ambapo jumla ya wananchi 2,905 walipatiwa huduma za msaada wa kisheria, wakiwemo wanaume 1,263 na wanawake 1,638. Kupitia kliniki hizo, migogoro 186 ilipokelewa, migogoro 14 ilitatuliwa papo kwa papo, huku migogoro 172 ikiendelea kushughulikiwa na watendaji husika.

Aidha, kupitia Kliniki za Sheria zinazoendeshwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wananchi 145 walihudumiwa na kusaidiwa kutatua migogoro mbalimbali ya kisheria ikiwemo migogoro ya ardhi, ajira, jinai, madai, mirathi na masuala ya familia, ambapo migogoro mingi ilipatiwa ufumbuzi papo kwa papo na mingine ikiendelea kufanyiwa kazi.

Utoaji wa Msaada wa Kisheria unaenda pamoja na uwepo wa Mawakili wabobezi na wanaoendana na kasi ya kiteknolojia katika utoaji wa huduma. Katika siku 100, Wizara imefanikiwa kutoa mafunzo kuhusu huduma za msaada wa kisheria kwa Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria 58 wakiwemo Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria 47 kutoka Sekretarieti za Mikoa na Mawakili wa Serikali 11 kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Wataalam hawa watasaidia kufikisha huduma za kisheria karibu na wananchi na pia kuongeza wigo wa mawakili watakao kuwa wanatoa msaada wa kisheria kwa wananchi wasiokuwa na uwezo pamoja na kusimamia mashauri ya wananchi yasiyokuwa na mgongano wa kimaslahi na serikali mahakamani.

Ajira kwa watumishi ni miongoni mwa vipaumbele alivyoahidi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha siku 100 za Uongozi. Wizara na taasisi zilizopo chini ya wizara zimepokea watumishi wapya 335 wa kada mbalimbali. Kati ya watumishi hao, watumishi 45 wameajiriwa Wizarani, watumishi 151 katika Mahakama ya Tanzania, watumishi 108 katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, na watumishi 31 katika Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Ajira hizi zinamanufaa makubwa katika kupunguza uhaba wa rasilimali watu katika sekta ya sheria, kuongeza ufanisi wa utoaji wa haki, na kuboresha upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi kwa wakati na kwa ufanisi zaidi.

Ujenzi wa Miundombinu ya Taasisi za Utoaji Haki ni sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Mahakama wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026). Lengo la mpango huo ni kuboresha na kusogeza huduma za Mahakama karibu na Wananchi ili kuwapunguzia gharama na muda wanaoutumia kupata huduma za mahakama. Katika kipindi cha siku 100 za utekelezaji wa shughuli za Serikali jumla ya Vituo Jumuishi tisa (9) vimeendelea kujengwa ambapo viwili (2) vimeshakamilika (Geita na Simiyu), Mahakama za Wilaya 13 zinaendelea kujengwa, Mahakama za Mwanzo 72 zimeendelea kujengwa ambapo mahakama za mwanzo 39 zimekamilika kwa asilimia 100.

Sambamba na hilo katika kipindi cha siku 100, Serikali iliendelea na ujenzi wa majengo ya Ofisi 10 za Mikoa ya Kimashtaka. Mikoa hiyo ni Njombe; Kinondoni; Temeke; Geita; Simiyu; Lindi; Singida; Kigoma; Songwe; na Kilimanjaro. Vilevile, katika kipindi husika Serikali ilianza ujenzi wa majengo ya Ofisi katika ngazi ya Wilaya kwa Wilaya sita (6) ambazo ni Kigamboni; Bahi; Mufindi; Manyoni; Hai; na Nzega.

Katika awamu ya kwanza ya Uongozi wa Rais Samia mageuzi makubwa yalionekana katika kuimarisha Mfumo wa Haki Jinai Nchini.Mageuzi haya ni pamoja na uundwaji wa Tume ya Haki Jinai iliyotoa mapendekezo 333 yanayolenga kuboresha utendaji wa taasisi za haki jinai.

Kati awamu ya pili ya uongozi wake, mkazo wa wazi umewekwa katika kuimarisha mifumo ya utoaji haki kama msingi wa mageuzi makubwa ya kitaifa. Katika kuimarisha ufanisi wa taasisi za haki jinai, Serikali imeandaa rasimu ya Muswada wa Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Haki Jinai ambao unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni baada ya kukamilika kwa taratibu za ndani ya Serikali. Kupitia muswada huo, jumla ya sheria 16 zimependekezwa kufanyiwa maboresho ili kuendana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia, pamoja na kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu na ufanisi wa mifumo ya haki jinai.

Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sheria ya Ushahidi, Sheria ya Mtoto, Sheria ya Taifa ya Mashtaka, Sheria ya Polisi na Askari Wasaidizi, Sheria ya Kuzuia Ugaidi, Sheria ya Ulinzi wa Watoa Taarifa na Mashahidi, pamoja na sheria nyingine muhimu zinazogusa moja kwa moja uendeshaji wa haki jinai nchini.

Mwelekeo huu wa kusisimua na ambao ukikamilika  utaweka misingi imara katika utawala bora, kufanikisha utekelezaji wa haki kwa wote  na ustawi wa jamii imara.

Serikali kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imemaliza na kushinda mashauri matatu (3) ya Usuluhushi. Kati ya mashauri hayo, mashauri mawili (2) ni ya usuluhishi wa kitaifa na shauri moja (1) ni la usuluhishi wa kimataifa. Kutokana na kumalizika kwa mashauri hayo, Serikali imeweza kukoa kiasi cha shilingi 57,776,283 na Dola za kimarekani milioni 336 Sawa na shilingi bilioni 829.58 kiasi ambacho Serikali ingekilipa endapo ingeshindwa mashauri hayo. Aidha, kiasi hiki cha Dola za kimarekani milioni 336 kimetokana na kumalizika kwa shauri la usuluhishi kwa njia ya majadiliano.

Katika kulinda maslahi ya Taifa, Mashauri ya Kisheria ya kimkakati yenye athari za kiuchumi na kijamii ni sehemu ya mafanikio katika siku 100 za Mhe. Rais Samia. Mathalani Ushindi wa Serikali katika shauri la Rufaa Na. 4/2023 katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki lililopinga ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga. Ushindi huo umewezesha kuendelea kwa utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati na kuimarisha shughuli za kiuchumi na maendeleo ya Taifa.

Siku 100 za Rais Samia, Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa mikataba mikubwa ya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa kufanya upekuzi wa kisheria wa mikataba hatua inayoonesha kuimarika kwa utawala wa kiuchumi. Hati za Makubaliano (MoUs) 121 zilifanyiwa upekuzi na maombi 13 ya ushauri wa kisheria kuhusu mikataba yalishughulikiwa. Kutokana na tathmini za kisheria zilizofanyika, mikataba nane (8) ilivunjwa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa, hatua iliyosaidia kuilinda Serikali dhidi ya athari za kisheria na kifedha.

Hatua hii inaendelea kuipa heshima Taifa la Tanzania kwa kusimamia usawa katika masharti ya mikataba, kuongeza ulinzi dhidi ya rasilimali za taifa na kuepuka udhalilishaji wa kiuchumi na kuimarisha mazingira ya biashara yanayokuza uchumi wa ndani.

Kwa ujumla, siku 100 za uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeweka msingi imara wa mageuzi ya sekta ya sheria. Kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, Serikali imeonesha kwa vitendo kuwa haki, usawa, na utawala wa sheria ni msingi wa maendeleo endelevu ya Taifa katika kulinda maslahi ya Taifa.

Haya ni mafanikio ya mwanzo,katika safari ya kujenga Tanzania yenye haki, amani,uwajibikaji, na maendeleo jumuishi kwa ustawi kwa wananchi wote.