Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Sisi Tuna Uhitaji Lakini Watoto Hawa Wana Uhitaji Zaidi: Makondo

Imewekwa: 05 Nov, 2023
Sisi Tuna Uhitaji Lakini Watoto Hawa Wana Uhitaji Zaidi: Makondo

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amesema Watoto wanaolelewa kwenye vituo mbalimbali vya yatima na wanaotoka katika mazingira hatarishi hapa nchini wana uhitaji mkubwa na changamoto nyingi kulinganisha na watu wengine, na kutoa wito kwa jamii kuendelea kuwakumbuka watoto hao mara kwa mara kwa kuwapelekea mahitaji mbalimbali ili kuwatia moyo kwenye maisha wanayopitia.

Bi. Makondo ameyasema hayo wakati yeye na watumishi wa Wizara hiyo walipotembelea kituo cha kulelea watoto wanaotoka kwenye mazingira hatarishi kiitwacho Safina Street Network kilichopo maeneo ya Ntyuka, tarehe 04 Novemba, 2023 Jijini Dodoma.

Katika tukio hilo Bi. Makondo na watumishi wa Wizara hiyo wameshiriki nao chakula cha mchana, kuimba nao nyimbo za kumtukuza Mungu kisha kuwakabidhi vitu mbalimbali vikiwemo sukari, chumvi, viatu vya wazi, nguo, sabuni unga na mafuta ya kupikia huku akiwataka watoto hao kushika mahusia ya Walimu wao na kusoma na kulishika Neno la Mungu.

“Sote ni wahitaji lakini Watoto hawa wana uhitaji zaidi, sote tuna changamoto lakini watoto hawa wana changamoto zaidi, sote tunashida lakini watoto hawa wanashida zaidi. Badhi ya watoto hawa hawana wazazi na wengine wana wazazi lakini wamewatelekeza, ni wajibu wa jamii kuwa nao na kuwafanya wenzetu,” alisema.

Kuhusu changamoto zozote za kisheria kwa watoto hao Bi. Makondo alisema, “tunawachukulia ninyi kama ndugu zetu, msisite kutwambia changamoto zenu zinazohusu ukosefu wa haki, unyanyasaji wa kijinsia au pale mtakapohitaji huduma za Serikali kwenye uhitaji wa sheria. Niwakumbushe kuwa Wizara ya Katiba na Sheria inatekeleza kampeni kubwa ya Msaada wa Sheria ya Mama Samia yenye lengo kutoa elimu na huduma ya sheria ili watanzani hasa wanyonge wapate haki.”

Naye Mratibu wa Kituo hicho chenye takribani watoto hamsini wa umri chini ya miaka saba hadi ishirini na tano wa kike na wa kiume Bw. Ebenezer Eliawira Ayo ameshukuru sana ujio huo akisema “matukio kama haya ya wageni kuwatembelea huwatia sana watoto moyo, huwapa faraja na huwa ni ukumbusho kuwa huko nje kuna maisha na kuna watu wanawajali, wanawapenda na wanawaombea.”

Mnufaika wa kituo hicho David Shaban anashukuru jinsi kituo hicho kilivyomtoa kwenye maisha ya mtaani, kimemlea na sasa anakitumikia kituo hicho kama mfanyakazi baada ya kuhitima elimu yake.