Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Takwimu za Matukio Muhimu ya Kibinadamu Ziboresha Utoaji wa Huduma za Kijamii – Dkt. Chana

Imewekwa: 25 Jun, 2024
Takwimu za Matukio Muhimu ya Kibinadamu Ziboresha Utoaji wa Huduma za Kijamii – Dkt. Chana

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa Taasisi za Serikali na Wadau wa Usajili wa matukio muhimu ya kibinadamu kutumia Takwimu za matukio hayo kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa umma.

Dkt. Chana ametoa wito huo alipokuwa anahutubia kufungua kikao kazi kilichoandaliwa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini – RITA kutathmini hali ya Utekelezaji wa Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano na kuzindua Taarifa ya kitakwimu ya usajili wa matukio muhimu ya kibinadamu, Juni 25, 2024 Jijini Dodoma.

“Matokeo ya taarifa hii yatumiwe vizuri na Taasisi za Serikali pamoja na wadau wa usajili wa matukio hayo kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa umma. Aidha, takwimu hizi zitumike kuwezesha uandaaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya kuendelea kuboresha usajili wa matukio hayo ili kutoa takwimu bora zaidi katika maeneo ya usahihi, ukamilifu na usajili kwa wakati.” Alisema.

Akitaja faida za usajili wa matukio muhimu ya kibinadamu amesema kunasaidia kupata taarifa sahihi za idadi ya watu ambazo ni muhimu katika kupanga mipango sahihi ya maendeleo kama programu za chanjo kwa watoto, huduma za afya na huduma za elimu. Takwimu hizo pia zinawawezesha viongozi wa ngazi zote kutoa huduma kwa kusaidia kutambua ni afua gani zinahitajika katika kukabiliana na changamoto katika maeneo yao.

Amezitaja faida zingine kuwa ni kuwawezesha watu kupata nyaraka muhimu za kisheria zinazoweza kulinda haki zao za msingi na haki za binadamu kama kuwa na jina, kitambulisho cha taifa, huduma za matibabu, elimu, uraia na kuwezesha huduma nyingine za msingi zinawafikia wananchi kwa uwiano sawa.

Dkt. Chana alitumia hafla hiyo kukumbusha azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona watoto wote wa umri chini ya miaka mitano wamesajiliwa ifikapo mwaka 2025 na wananchi wote wa Tanzania Bara wamesajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa ifikapo mwaka 2030. Hivyo akatoa wito kwa RITA kuendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma zake zote na kuandaa mpango kazi utakaoonesha jinsi itakavyoongeza usajili wa matukio yote muhimu ya binadamu katika kulifikia lengo hilo.

Awali akitoa salaam za Bodi ya Ushauri ya RITA na baadaye kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Amina Msengwa amemhakikishia Waziri kuwa Bodi itaendelea kufuatilia na kuisimamaia RITA katika kutekeleza majukumu yake ya usajili wa matukio muhimu ya kibinadamu kwa kadri ya malengo ya Serikali.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Kisheria kwa Umma Bw. Abdulrahman Mshamu akitoa salaam za Wizara kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria amepongeza ubora wa kazi iliyofanywa na RITA kutoa takwimu za Matukio Muhimu ya Kibinadamu, “kazi hii ni nzuri na ukiunganishwa kwenye mnyororo wa utendaji wa kazi za Serikali utaiwezesha kutekeleza mipango yake kwa urahisi kwani kama inavyosemwa kama huna takwimu au taarifa ni ngumu sana kuweka mipango endelevu.”