TANZANIA INA SHERIA IMARA ZA KULINDA NA KUSIMAMIA RASILIMALI ZA NCHI
Tanzania ina mfumo imara wa kisheria unaolenga kulinda, kuhifadhi na kusimamia rasilimali za nchi, hususan rasilimali za bahari na mazingira, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri Asili na Maliasili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, DCP Neema M. Mwanga, alipokuwa akizungumza katika banda la Wizara hiyo wakati wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP 12), unaofanyika katika Ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
DCP Mwanga amesema Serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa sheria na sera zinazolenga kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa na kusimamiwa kwa uendelevu, huku ikihakikisha wananchi wanapata manufaa kutokana na fursa zinazotokana na rasilimali hizo.
Amesema miongoni mwa sheria zinazochangia katika ulinzi na usimamizi wa rasilimali za bahari ni Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu, Sheria ya Uvuvi pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA), ambazo zinaweka misingi ya kudhibiti shughuli zinazoweza kuathiri mazingira na mifumo ya ikolojia ya bahari na maeneo ya pwani.
Aidha, amesema Serikali imeweka pia mifumo ya kisheria inayolenga kuhakikisha wananchi wanashiriki na kunufaika na fursa zinazotokana na rasilimali za nchi, ikiwemo kupitia Sheria ya Ugawanaji Sawia wa Uwezeshaji wa Wananchi.
Ameeleza kuwa kupitia ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya kimataifa kama COP 12, Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kutoa uelewa kuhusu mifumo ya kisheria iliyowekwa na Serikali katika kulinda rasilimali za nchi na mazingira ya bahari.
Amesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa na kusimamiwa kwa ufanisi, ili ziendelee kuwa na manufaa kwa wananchi na vizazi vijavyo.