Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

ULEGA ATAKA WANANCHI WENGI ZAIDI WASAIDIWE KUPATA MSAADA WA KISHERIA

Imewekwa: 08 Oct, 2026
ULEGA ATAKA WANANCHI WENGI ZAIDI WASAIDIWE KUPATA MSAADA WA KISHERIA

WAZIRI wa Katiba  na  Sheria Mhe. Abdallah Ulega, amesema matamanio yake makubwa ni kuona wananchi wengi zaidi wakipata huduma za  Msaada wa  kisheria  kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia  Awamu ya Pil ili wasipoteze haki zao.

Waziri Ulega ameyasema hayo Oktoba 7, 2026  katika Ofisi za Wizara  Mtumba jijini Dodoma, wakati akizungumza na Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara. 

“Nimekua  nikifuatilia utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia na kwa kweli nikiri hadi sasa mmefanya kazi kubwa sana ya kusaidia wananchi kisheria, ninatamani awamu hii wananchi wengi zaidi wapate haki yao “ alisema.  

Aidha, Mhe. Ulega amesisitiza kuwa anathamini kazi na matokeo pamoja na kuiomba menejimenti ya wizara kumpa ushirikiano utakaowezesha kufanya kazi kwa umoja na kujituma ili kuweza kupata matokeo yaliyotarajiwa na serikali na wananchi pia.

“Hii ni dream team ambayo Serikali imeileta hapa ili kupata matokeo, hivyo lazima tufanye kazi kwa bidii kwa kuzingatia Dira, Ilani na miongozo iliyowekwa ili kuweza kufikia matokeo yanayotarajiwa,” alisema Mhe. Ulega.

“Mimi ninapenda kufanya kazi na ninapenda matokeo pia, hivyo ninaamini mtanipa ushirikiano ili tufanye kazi kwa umoja na kujituma tuweze kupata matokeo na kuendeleza yote mazuri ambayo mnayatekeleza,” alisisitiza Mhe. Ulega.

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama  Ilianzishwa na  Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo wananchi wenye changamoto za kisheria hufikiwa na wataalamu na kupatiwa huduma za Msaada wa Kisheria ikiwemo uwakilishi Mahakamani na elimu ya  kisheria bila malipo.