Tanzania Imeweka Mikakati ya Kupambana na Umaskini – Pindi Chana

Na Lusajo Mwakabuku – WKS Geneva
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali ya Tanzania imeweka mikakati mbalimbali katika kuhakikisha inaondoa wimbi la umaskini uliokithiri katika jamii ambao hupelekea maskini kupata Haki za kibinadamu kwa kiasi kidogo au kutozipata kabisa.
Waziri Chana amesema hayo leo tarehe 02/07/2024 alipokuwa akichangia mjadala unaohusu umaskini uliokithiri na jitihada za kuutatua katika kikao cha 56 cha Baraza la Haki za Binadamu kinachoendelea katika Ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Geneva, Switzerland.
Waziri Chana amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafuata msingi wa maendeleo unaozingatia haki za binadamu, maisha bora, utulivu wa amani na umoja, utawala bora, kuwa na jamii iliyoelimika na yenye uchumi imara wenye ushindani ni baadhi ya sifa kuu za Dira ya Maendeleo ya 2025.
“Pia tuko katika mchakato wa kuendeleza DIRA yetu ya maendeleo ya 2050 ambayo ni mchakato shirikishi unaowaleta pamoja Watendaji wa Serikali na Wasiokuwa wa Serikali ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika ajenda ya maendeleo”. Aliongeza Pindi Chana
Waziri Chana alihitimisha mchango wake kwa kuelezea jinsi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyofanya Sensa ya Kitaifa ya Watu na Makazi mwaka 2022 ikiwa ni nyenzo ya kimkakati itakayotumika wakati wa kuandaa mpango wa maendeleo wa DIRA 2050 unaolenga kukomesha umaskini na kukuza haki za binadamu kwa kuzingatia Maendeleo Endelevu.