Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tanzania na UNDP Zakubaliana Kuimarisha Sekta ya Sheria

Imewekwa: 23 Apr, 2024
Tanzania na UNDP Zakubaliana Kuimarisha Sekta ya Sheria

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Bw. Shigeki Komatsubara na kukubaliana ufadhili wa masuala mbalimbali katika kuimarisha Sekta ya Sheria na utoaji haki.

Mazungumzo hayo yamefanyika tarehe 23 Aprili, 2024 ofisi za Wizara Mtumba Dodoma na kuhudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Khatibu Kazungu na viongozi wengine wa Wizara.

Akiongea katika kikao hicho Dkt. Chana ameshukuru utayari wa UNDP kufadhili maboresho hayo ya sekta ya sheria na kuyataja baadhi ya maeneo yanayohitaji ushirikiano kwenye Wizara na Taasisi zake kuwa ni pamoja na ufadhili wa Mpango wa kusajili watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, Utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, Uimarishaji wa mifumo ya TEHAMA, Uhuishaji wa taarifa mbalimbali zitakazosaidia kutoa maamuzi, Mradi wa usimamizi wa utajiri na maliasilia za nchi na Mafunzo ya kitaalamu.