Tanzania ni Nchi ya Mfano kwa Kupokea na Kuwahifadhi Wakimbizi.

Na Lusajo Mwakabuku – WKS GENEVA
Tanzania imetajwa kuwa nchi ya mfano katika kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi toka enzi za Rais wa Awamu ya Kwanza Hayati Julius Kambarage Nyerere.
Hayo yameelezwa na Kamishna Mkuu Msaidizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR bwana Raouf Mazou, alipofanya mazungumzo na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana tarehe 04/07/2024 Ofisini kwake yalipo Makao Makuu ya Shirikika hilo Geneva, Switzerland.
Kamishna Mazou aliongeza kuwa Tanzania ukilinganisha na nchi nyingine imekuwa ikipokea wakimbizi na kuwapatia mahitaji muhimu na pia akatumia nafasi hiyo kugusia suala la elimu kwamba watoto wanaoishi katika maeneo ya wakimbizi waweze kupatiwa elimu bora na itakayoweza kuwasaidia kuendelea kimasomo mara wanaporudi nchini mwao.
Kwa upande wake Waziri Chana alisema Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza uhamasishaji katika maeneo ambayo wanaingilia wakimbizi kama vile Kigoma kama ambavyo Mwalimu Nyerere alisema kuwa tofauti ni mipaka ila waafrika ni wamoja na pia akatoa mfano wa Rais Kabila ambaye anaye alikuwa mkimbizi nchini Tanzania na akaweza kurudi nchini kwao na kuwa kiongozi.
Akijibu suala la elimu, Waziri Chana alisema akirudi nchini atawasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani pamoja na Waziri wa Elimu kuona ni namna gani wataweza kufanikisha hilo na pia akatumia nafasi hiyo kumwomba Kamishna Mazou kuangalia nafasi zozote za ushirikiano katika masuala ya uwezeshaji kwa watu wanaowashughulikia wakimbizi nchini Tanzania.