TANZANIA YASHIRIKIANA NA MATAIFA YA NJE KUIMARISHA MFUMO WA HAKI JINAI
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imepata fursa ya kubadilishana uzoefu na mataifa mbalimbali duniani kuhusu masuala ya kuzuia uhalifu na namna bora ya kuimarisha mfumo wa haki jinai na utawala wa sheria.
Tanzania imepata fursa hiyo kupitia “Kongamano la Umoja wa Mataifa la Kuzuia Uhalifu na Haki Jinai” lililofanyika kuanzia tarehe 25 Septemba hadi 1 Oktoba, 2026 Abu Dhabi UAE ambapo nchi wanachama kutoka maeneo mbalimbali duniani zilipata nafasi ya kujadili mikakati madhubuti ya kupambana na changamoto za kiusalama zikiwemo rushwa, ugaidi, biashara haramu ya binadamu, dawa za kulevya, pamoja na uhalifu unaokua kwa kasi wa mtandaoni.
Kupitia ushiriki wa kongamano hili, Tanzania inapata fursa ya kuimarisha matumizi ya mifumo ya kisasa ya TEHAMA na mifumo ya pamoja ya taarifa za haki jinai nchini (Integrated Criminal Justice Information Systems), ili kurahisisha upatikanaji wa data na ushahidi kwa wakati jambo litakaloboresha utoaji wa haki, ulinzi wa waathirika wa uhalifu hususan makundi yaliyo katika mazingira hatarishi pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwenye uchunguzi wa makosa ya jinai.
Aidha, kongamano hili litasaidia kuimarika kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na nchi nyingine wananchama, hatua itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na uhalifu unaovuka mipaka (transnational crimes).
Kongamano la Umoja wa Mataifa la Kuzuia Uhalifu na Haki ya Jinai ni jukwaa kuu duniani linalokutanisha serikali, wataalamu na wadau wa sheria kila baada ya kipindi fulani ili kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia uhalifu na kuimarisha mifumo ya mahakama na usalama duniani.