Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

TANZANIA YAAHIDI  KUENDELEZA USHIRIKIANO NA UN KUFIKIA MAENDELEO ENDELEVU

Imewekwa: 24 Oct, 2026
TANZANIA YAAHIDI  KUENDELEZA USHIRIKIANO NA UN KUFIKIA MAENDELEO ENDELEVU

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa (UN) katika kukuza amani, kuimarisha taasisi za kitaifa na kuharakisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (Mb.), aliyemwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, katika maadhimisho ya miaka 81 ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 23, 2026.

Mhe. Ulega amesema Tanzania inathamini uhusiano wake na Umoja wa Mataifa, ambao umekuwa na mchango muhimu katika kuimarisha taasisi za kitaifa, kusaidia programu za maendeleo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na kukuza ushirikiano wa kimataifa na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano huo kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa  na kuhakikisha unaleta matokeo yenye manufaa kwa wananchi.

Akizungumzia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Waziri Ulega amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, Umoja wa Mataifa na wadau wa maendeleo katika kuwekeza kwa wananchi, kuimarisha taasisi, kukuza ubunifu na kupanua fursa za kiuchumi na kubainisha kuwa uwezeshaji wa wanawake na vijana kupitia elimu, mafunzo ya ujuzi, ujasiriamali, upatikanaji wa mitaji na fursa za ajira ni muhimu katika kufanikisha maendeleo jumuishi na endelevu.

Amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja wa kitaifa, maridhiano na utawala jumuishi, akieleza kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kujenga taifa lenye ustawi na ustahimilivu na kuongeza kuwa Tanzania inaendelea kuunga mkono ushirikiano wa kimataifa, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani na mageuzi ya Umoja wa Mataifa yatakayoongeza ufanisi, uwakilishi na ushirikishwaji wa nchi wanachama, hususan Afrika na nchi zinazoendelea.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Miaka 81 ya Umoja wa Mataifa: Kujenga Mustakabali wa Amani, Utu na Uendelevu kwa Wote.” (81 Years of United Nations: Building a Future of Peace, Dignity, and Sustainability for All) ikilenga kusisitiza wajibu wa pamoja wa mataifa katika kujenga dunia yenye amani, maendeleo jumuishi na endelevu yenye manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa hutoa fursa ya kutafakari mafanikio ya Umoja ya Mataifa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1945, kuthibitisha tena misingi na madhumuni ya Mkataba wa kuanzishwa kwa umoja huo, pamoja na kuhuisha dhamira ya pamoja ya kushirikiana katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia