Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

TANZANIA YAELEZEA MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA  HAKI  ZA KIJAMII BARAZA LA UMOJA  WA  MATAIFA

Imewekwa: 24 Jun, 2026
TANZANIA YAELEZEA MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA  HAKI  ZA KIJAMII BARAZA LA UMOJA  WA  MATAIFA

Tanzania imeendelea kuonesha dhamira yake ya kulinda, kuheshimu na kuendeleza haki za binadamu kwa kuwasilisha mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika sekta za afya, elimu, upatikanaji wa taarifa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Kikao cha 62 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea mjini Geneva, Uswis.

Kikao hicho kinachofanyika kuanzia Juni 15 hadi Julai 7, 2026, kimeipa Tanzania fursa ya kueleza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za kijamii na kufurahia haki zao za msingi kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

Akiwasilisha taarifa kuhusu uhuru wa kupata taarifa, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Geneva, Dkt. Abdallah Possi, alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali na huduma za mawasiliano ili kupanua upatikanaji wa taarifa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Alieleza kuwa uwekezaji huo umechangia kuimarika kwa huduma za intaneti na mawasiliano, hatua inayowezesha wananchi kupata taarifa kwa wakati, kushiriki katika majukwaa ya kidijitali na kunufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kwa upande wa elimu, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Beatrice Mpembo, alibainisha kuwa Serikali inaendelea kutekeleza kwa vitendo haki ya elimu kupitia sera ya elimu bila malipo katika ngazi za msingi na sekondari.

Alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya elimu, ikiwemo shule mpya katika maeneo mbalimbali ya nchi, pamoja na kuajiri walimu wenye sifa na weledi ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na yenye ubora unaokidhi mahitaji ya Taifa.

Uwasilishaji wa taarifa hizo umeonesha namna Tanzania inavyoendelea kuchukua hatua madhubuti katika kukuza ustawi wa wananchi na kuimarisha mazingira yanayowawezesha kufurahia haki zao za msingi, huku ikiendelea kutekeleza wajibu wake wa kimataifa katika masuala ya haki za binadamu.

Mkutano huo unaendelea kutoa jukwaa muhimu kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kubadilishana uzoefu na kuwasilisha maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa haki za binadamu kwa manufaa ya wananchi wao.