Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tanzania yapongezwa kwa kuimarisha Demokrasia nchini

Imewekwa: 29 Mar, 2023
Tanzania yapongezwa kwa kuimarisha Demokrasia nchini

Na Farida Khalfan & Lusajo Mwakabuku - WKS

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  imepongezwa na Serikali ya Marekani kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha demokrasia nchini. Pongezi hizo zimetolewa leo 29/03/2023 katika kikao cha 52 cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu kinachoendelea Geneva – Switzerland ambacho kilianza Februari 27 na kitafikia ukomo Aprili 4, 2023.

Tanzania imepata pongezi hizo kufuatia jitihada kubwa ilizochukua katika kuimarisha demokrasia ikiwa ni pamoja na kuwezesha Vyombo vya Habari kuwa huru, kuvifungulia Vyombo vya Habari vilivyofungiwa, kujenga mahusiano chanya na Viongozi wa Vyama vya Siasa vya Upinzani ikiwa ni pamoja kuruhusu mikutano ya kisiasa nchini hali iliyochangia  kukuza na kuimarisha demokrasia nchini.

Ikumbukwe kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishiriki kikamilifu Vikao hivi vya Haki za Binadamu na Watu na Februari Mwaka huu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro alishiriki katika kikao hicho kwa njia ya mtandao ambapo aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Haki za Binadamu nchini ikiwemo za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii.

Aidha, Tanzania imeshiriki katika vikao vya awali ambapo maelezo ya haki za vijana, makazi salama, haki ya kupata chakula, watoto, watu wenye ualbino, watu wenye ulemavu na haki ya maendeleo yamewasilishwa.

Mbali na hayo, Tanzania imeahidi kuendelea kutekeleza wajibu wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu chini ya mikataba ya haki za binadamu iliyoridhia kwa kuchukua hatua za kisera, kisheria, kitaasisi na kiutawala kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo.