Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tanzania Yapongezwa kwa Kuweka Mifumo Shirikishi Katika Kuimarisha Haki za Binadamu na Watu

Imewekwa: 23 Oct, 2023
Tanzania Yapongezwa kwa Kuweka Mifumo Shirikishi Katika Kuimarisha Haki za Binadamu na Watu

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutengeneza mifumo shirikishi yenye lengo la kukuza na kuimarisha haki za binadamu na watu nchini.

Mhe. Jaji Mwaimu ametoa pongezi hizo tarehe 23 Oktoba 2023 wakati akihutubia wajumbe wa Kikao cha Kawaida cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachoendelea jijini Arusha.

Mhe. Jaji Mwaimu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanikiwa kuweka mifumo shirikishi inayowezesha wadau mbalimbali kujadili mambo muhimu ya kitaifa ikiwemo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ikiwa ni jitihada za Serikali za kuendelea kuimarisha na kuboresha usimamizi wa haki za binadamu na watu.

Akizitaja  hatua za Serikali zinazodhihirisha mwenendo mzuri wa kuimarika na kustawi kwa haki za bianadamu na Watu nchini kuwa ni pamoja na  kuwekwa mfumo shirikishi  wa kujadili mambo muhimu ya Kitaifa na kuimarika kwa demokrasia ambapo Mhe. Rais Samia aliunda Kamati Maalum kwa ajili ya kutathmini mwenendo mzima wa masuala ya siasa nchini.

“Tunapenda katika mkutano huu kuweka msisitizo katika masuala machache ambayo Tume imeona kwamba yana mwelekeo chanya na yamejipambanua kutokana na umuhimu wake. Kwanza ni hatua ya Serikali ya Tanzania ya kuweka mfumo shirikishi wa kujadili mambo muhimu ya kitaifa. Mfano hivi karibuni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na Vyama vya Siasa nchini walikaa pamoja jijini Dar es Salaam kujadili taarifa ya kamati Maalum iliyoundwa ba Mhe. Rais Dkt. Samia kwa ajili ya kukuza mwenendo mzima wa masuala ya siasa ikiwemo demokrasia ya Vyama Vingi.

Pia amepongeza hatua ya kuzinduliwa kwa Kampeni ya miaka mitatu ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria ambayo mpaka sasa imetekelezwa kwenye mikoa mitano na kuwafikia zaidi ya wananchi 2,870 waliopo kwenye maeneo 39 ya vizuizi na zaidi ya wananchi 361,740 waliopo uraiani wamehudumiwa kwa ukamilifu na kufaidika.

Amesema, miongoni mwa waliofaidika na Kampeni hii ni wahamiaji raia wa Ethiopia zaidi ya 80 ambao walirejeshwa nchini kwao baada ya kuwa vizuizini kwa changamoto za uhamiaji.

Mhe. Jaji Mstaafu Mwaimu pia aliutaja mchakato ulioanzishwa na Mhe. Rais Dkt. Samia wa kupitia upya mfumo wa Taasisi zinazoshughulikia masuala ya Haki Jinai kuwa ni wenye tija kubwa  na wa kuigwa kwenye kuimarisha  Nyanja za haki za binadamu na watu nchini.

“Tume imeona suala la Mhe. Rais Dkt. Samia la kuanzisha mchakato wa kupitia upya mfumo wa taasisi zinazoshughulikia masuala ya haki jinai kuwa ni jambo kubwa na lenye tija. Mchakato huu ambao unalenga kufanya mapitio ya mnyororo mzima wa haki jinai kwa kushughulikia dosari za upatikanaji wa haki za binadamu utaleta tija na kuimarisha haki za binadamu hapa nchini pale utakapokamilika,” alisisitiza Mhe. Jaji Mwaimu.

Pia Tume hiyo imepongeza utayari wa Serikali wa kuanza kuandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Biashara na Haki za Binadamu ambao ukikamilika utawezesha kuingiza katika mfumo Kanuni za Umoja wa Mataifa za masuala ya Haki za Binadamu na Biashara na kuwahakikishia Watanzania kufanya shughuli za biashara kwa namna inayozingatia na kuhifadhi haki za binadamu.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni Idara huru ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2001 ambayo pamoja na mambo mengine husimamia utekelezaji wa haki za binadamu na watu nchini.

Kikao cha Kawaida cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kilifunguliwa rasmi tarehe 20 Oktoba 2023 na kinatarajiwa kumalizika tarehe 09 Novemba, 2023.