Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

TUACHE MUHALI, TUSEME UKWELI NA TUCHUKUE HATUA KUPINGA VITENDO VYA UKATILI- RAIS MWINYI

Imewekwa: 13 May, 2025
TUACHE MUHALI, TUSEME UKWELI NA TUCHUKUE HATUA KUPINGA VITENDO VYA UKATILI- RAIS MWINYI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, kuwalinda watoto na wanawake ili kulinda kizazi kijacho.

Dkt. Mwinyi ametoa rai hiyo leo tarehe 10 Mei 2025 katika uwanja wa Azimio Mtende wakati akizindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika mkoa wa Kusini Unguja ambapo ameongeza kuwa migogoro ni chanzo cha uvunjifu wa Amani katika jamii.

“Mapambano dhidi ya udhalilishaji kijinsia si ya mtu mmoja ni ya wote, Tuache muhali, tuseme ukweli na tuchukue hatua, kuwalinda watoto na wanawake dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ni kukilinda kizazi kijacho”, amesisitiza Dkt. Mwinyi

Dkt Mwinyi ameongeza kuwa jukumu la kukomesha ukatili na unyanyasaji wa kijinsia sio la mtu mmoja bali jamii nzima ikiwa ni pamoja na familia, viongozi wa dini na asasi mbalimbali huku akipongeza kampeni kwa kutoa elimu na utatuzi wa migogoro katika maeneo ya ukatili wa kijinsia, mirathi, na migogoro ya ardhi ambayo ndio chanzo cha uvunjivu wa amani.

Aidha Dkt. Mwinyi amesema kuwa serikali inaendelea kuimarisha mahakama na Taasisi zote zinazohusika na utoaji haki ili kuhakikisha upatikanaji wa haki na huduma za kisheria zinaimarika na kusogezwa karibu na wananchi kwa lengo la kushughulikia changamoto zao.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa kampeni ya Msaada wa Kisheria kwa upande wa Tanzania Bara Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini amesema jumla ya wananchi 2,774,495 wakiwemo wanawake 1,390,535 na wanaume 1,381,960 wamepatiwa huduma za Msaada wa Kisheria tangu kuzinduliwa kwa kampeni hiyo mwezi Machi 2023.

Mhe. Sagini ameongeza kuwa migogoro 5,704 imetatutliwa kati ya migogoro 23,399 ya muda mrefu iliyoibuka huku migogoro 18,987 ikiwa katika hatua mbalimbali za utatuzi na utekelezaji wa kampeni tayari umefikia Mikoa 25, halmashauri 180 na vijiji/mitaa 8702 ya Tanzania bara huku mkoa uliosalia wa Dar es Salaam ukitarajiwa kukamilika mwezi Juni 2025.