Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tuishauri Serikali Tusikae Kimya - Sagini

Imewekwa: 03 Jul, 2024
Tuishauri Serikali Tusikae Kimya - Sagini

Hyasinta Kissima - WKS Dodoma

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kusimamia  jukumu lake la msingi la kuishauri Serikali katika masuala yote ya Kisheria ndani na Nje ya Nchi ambapo ameelekeza Ofisi hiyo kuendelea kusimamia haki, uadilifu na kuishauri Serikali kwa hekima na heshima.

Naibu Waziri Sagini aliyasema hayo Julai 2, 2024  jijini Dodoma, wakati akizungumza katika kikao na Menejimenti na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mhe. Sagini amesema kuwa  katika uandaaji wa Sheria inapoonekana kunaweza kuibuka ukakasi katika utekelezaji wake ni  vyema Ofisi hiyo ikatoa taarifa mara moja kwa Viongozi na kushauri ipasavyo   ili kuzuia madhara kwa Serikali na Wananchi.

"Ninyi ni Taasisi ya Kikatiba. Tunaona jitihada kubwa zinazofanywa katika kuimarisha msaada wa Kisheria ikiwa ni pamoja na kuendelea kusimamia nidhamu ya Mawakili wa kujitegemea kwani wapo ambao wanawaonea Wananchi. Panapotokea jambo ambalo mnaona Kisheria linaweza kuleta maneno ni vyema mkaliwasilisha na mkatumia taaluma yenu kushauri badala ya kukaa kimya. Mnafanya kazi kubwa sana endeleeni kutimiza wajibu wenu  kwa maslahi makubwa ya Nchi yetu na pia endeleeni kuimarisha umoja na mshikamano pahala pa kazi." Alisema Naibu Waziri Sagini.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu amesema kuwa, Wizara kwa sasa imeanza kuandaa maandiko ya miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa kuwajengea uwezo Wanasheria ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na moja kati ya mambo yaliyokusudiwa kupitia mradi huo ni kuimarisha utendaji kazi  wa Wanasheria katika maeneo mbalimbali yanayoibuka kwenye taaluma hiyo na ambayo mara nyingi hayapatikani katika Vyuo hapa Nchini.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo kwa Naibu Waziri, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Prof Kennedy Gastorn amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha mwaka 2023/2024, imepata mafanikio kadha wa kadha ikiwa ni katika  kufanikisha Urekebu wa Sheria kuu 446 ili toleo la Sheria lililofanyiwa urekebu kwa mwaka 2023 liweza kutoka, kufanya tafsiri ya Sheria 300, kuhakiki Sheria ndogo 1228, kufanya upekuzi kwa hati za makubaliano 34, kutoa maoni 1707 kwenye Wizara na Taasisi na kufanikisha miswada 19 iliyoandaliwa ambapo miswada 17 ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Sheria.