Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tukitekeleza Kazi kwa Kasi Hii Tutaelewana: Dkt. Chana

Imewekwa: 18 Oct, 2023
Tukitekeleza Kazi kwa Kasi Hii Tutaelewana: Dkt. Chana

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amepokea taarifa za utekelezaji za Robo Mwaka ya Mwisho kwa mwaka wa fedha 2022/23 na Robo Mwaka ya Kwanza kwa mwaka 2023/24 kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara na kuzipongeza kwa kazi nzuri na utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo kwa wakati.

Mhe. Chana ametoa pongezi hizo wakati yeye na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul walipokutana na Watendaji kutoka Taasisi hizo na Menejimenti ya Wizara tarehe 17 Oktoba, 2023 kwenye ofisi za Wizara Mtumba Dodoma.

“Kazi mlizofanya zinatoa alert, ni taarifa chunguzi za ukweli na zinazoonesha haki imekuwa ikitendeka,” alisema Mhe. Waziri na kwa namana ya pekee amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya sheria na kuahidi kwamba Wizara yake itaendelea kusimamia utoaji haki na kutekeleza maono ya Mhe. Rais ya kutaka haki sawa kutolewa na kwa wakati.

Katika kikao kazi hicho pia Mhe. Waziri alipokea Mswada wa marekebisho mbalimbali kwenye sekta ya sheria yenye Sehemu Ishirini na nne yanayolenga kuweka mazingira wezeshi katika kuendelea kutekeleza majukumu kwa wakati, kuzuia matumizi mabaya ya mali ya umma, kuondoa changamoto ya tafsiri kwa baadhi ya sheria na hivyo kuondoa mkanganyiko katika kutekeleza sheria hizo ili kuboresha utoaji wa haki na hivyo kuongeza ufanisi wa kazi.

Katika hatua nyingine Mhe. Waziri alikutana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi na kujadili masuala mbalimbali ya kuboresha ya sekta ya sheria na utoaji haki.

Akichangia katika kikao kazi hicho Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Gekul aliitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora itumie sehemu ya utawala bora kuandaa mafunzo kwa viongozi wa ngazi za chini za utawala wakati nchi inajiandaa na Uchaguzi wa Serikali za Mtaa mwakani. Aidha, Mhe. Gekul ameitaka Tume hiyo kuwa na mkakati wa kuwafikia wananchi wa chini kabisa. “Kiu yangu ni kuona mna Maafisa kwenye kila mkoa ili kuwarahisishia wanachi kuwafikishia kero zao,” alisema.

Pamoja na Menejimenti ya Wizara, Taasisi zilizoshiriki kikao kazi hicho ni pamoja na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mahakama, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na RITA na Tume ya Kurekebisha Sheria.