Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

TUME YA HAKI ZA BINADAMU YAZINDUA BUSTANI YA MITI DODOMA

Imewekwa: 05 Jun, 2026
TUME YA HAKI ZA BINADAMU YAZINDUA BUSTANI YA MITI DODOMA

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imezindua rasmi Bustani ya Miti Nkuhungu jijini Dodoma, mradi wa mazingira ulioanzishwa mwaka 2022 kwa lengo la kuimarisha uhifadhi wa mazingira, kukuza ustawi wa jamii na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, Mgeni Rasmi Bi. Nkasori Sarakikya Juni 4, 2026 amesema kuwa uhifadhi wa mazingira ni moja ya nguzo muhimu za Dira ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa kinara katika matumizi endelevu ya rasilimali za asili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Bi. Sarakikya ameongeza kuwa haki za binadamu na mazingira ni mambo yanayoendana, huku juhudi za upandaji miti zikichangia kuboresha mazingira, afya na ustawi wa jamii kwa kizazi cha sasa na vijavyo.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Patience Ntwina, amesema kuwa Bustani hiyo sasa imefikisha miti 500 baada ya miti 30 kupandwa wakati wa hafla hiyo, ikiongezeka kutoka miti 470 iliyokuwepo awali na kwamba eneo hilo pia linatarajiwa kuendelezwa kuwa ukumbi maalum wa matukio mbalimbali na kupambwa kwa maua ya kuvutia ili kuongeza thamani ya mazingira na kijamii.

Hata hivyo akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mtaa wa Salama Mwenyekiti wa mtaa huo Bw. Habasi Mwijuki ameeleza kuwa bustani hiyo imeboresha mandhari ya eneo hilo na kuongeza fursa za kijamii na kielimu ambapo pia alitumia fursa hiyo kuomba kuwekwa vimbweta katika bustani hiyo ili wanafunzi wa Shule ya Msingi Nkuhungu waweze kuitumia kama sehemu ya kujisomea.

Uzinduzi huo umefanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni ambapo Tume hiyo imeambatanisha bustani hiyo na kaulimbiu ya Mazingira safi na salama ni haki ya msingi ya Binadamu.